LONDON :Uingereza ilijadili kumpinduwa Saddam
1 Mei 2005Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair leo amesema kwamba Uingereza ilijadili na Marekani juu ya suala la kubadili utawala nchini Iraq miezi minane kabla ya kuvamiwa kwa nchi hiyo hapo mwezi wa Machi mwaka 2003.
Lakini waziri mkuu huyo ambaye anakabiliwa na uchaguzi Alhamisi ijayo ambapo vita hivyo vya Iraq vinaweza kumgharimu kura amekanusha taarifa kwamba serikali yake ilikuwa imeamuwa na mapema kumpinduwa Saddam Hussein.
Kauli yake hiyo inakuja kufuatia waraka uliovujishwa kwa gazeti ambao unasema kwamba Blair na Rais George W Bush wa Marekani walikuwa wameazimia kumpinduwa kiongozi huyo wa Iraq mapema mwezi wa July mwaka 2002.
Blair amekaririwa akisema kwamba alizungumzia suala hilo la kubadili utawala iwapo itakuwa haiwezekani kumlazimisha Saddam kutekeleza sheria ya kimataifa .