LONDON : Sheikh wa itikadi kali apigwa marufuku kurudi Uingereza
13 Agosti 2005Serikali ya Uingereza imempiga marufuku sheikh wa Kiislam mwenye itikadi kali kurudi tena nchini humo.
Sheik huyo mzalia wa Syria Omar Bakri Mohammed ambaye amekuwa akiishi nchini Uingereza kwa miaka 20 iliopita hivi sasa yuko nchini Lebanon.Msemaji wa serikali amesema kwamba kuwepo kwa Bakri nchini Uingereza hakusaidii kuleta tija kwa wananchi.Hatua hiyo inakuja wakati afisa mwandamizi wa masuala ya sheria nchini Uingereza akitetea mipango ya kumrudisha kwao sheikh mwengine wa Kiislam wa itikadi kali pamoja na wageni wengine tisa wanaotuhumiwa kuwa tishio kwa usalama wa taifa.
Jordan imesema hapo jana kwamba itaiomba Uingereza kumrudisha nchini humo mmojawapo ya watu hao inaowashikilia ambaye ni sheik Omar Mahmoud Othman Abu Omar ambaye pia anajulikana kwa jina la Abu Qatada ambaye serikali ya Uhispania huko nyuma iliwahi kumwelezea kuwa ni balozi wa kidini wa Osama bin Laden barani Ulaya.