LONDON: Polisi waendelea kuwahoji washukiwa 23
14 Agosti 2006Polisi nchini Uingereza wanaendelea kuwahoji washukiwa 23 na kusaka nyumba katika uchunguzi wao wa njama ya kuziripua ndege kumi za abiria kutoka Uingereza kuelekea Marekani.
Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa jamii ya waislamu kuhusu kukamatwa kwa watuhumiwa hao. Lakini mmoja wao amesisitiza kukamatwa kwao hakuna uhusiano wowote na uislamu.
´Kilichosababisha watu hawa kukamatwa na iwapo kutapatikana ushahidi ulio wazi, basi hao ni wahalifu na wala sio magaidi wa kiislamu. Uislamu hauna uhusiano wowote na kukamatwa kwao.´
Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza, John Reid, amesema bado kuna uwezekano mkubwa wa mashambulio kufanywa. Ameongeza kusema njama nne zimevunjwa tangu mashambulio ya Julai saba yaliyofanywa mjini London mwaka jana.
Waziri Reid amesema polisi pia wanachunguza njama zaidi ya 20 za ugaidi.