LONDON : Mmoja mbaroni kuhusiana na miripuko Uingereza
13 Julai 2005Polisi ya Uingereza imesema imewatambuwa watu wanne wanaotuhumiwa na uripuaji wa mabomu wiki iliopita mjini London uliouwa watu 52 na kujeruhi wengine 700 shambulio ambalo ni baya kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini Uingereza tokea kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Mkuu wa tawi la kupiga vita ugaidi katika polisi ya jiji la London Peter Clarke amewaambia waandishi wa habari mjini London kwamba wana ukanda wa picha ya televisheni unaoonyesha wanaume hao wakiwasili katika kituo cha treni cha King Cross kabla ya miripuko hiyo.Clarke amesema wanaamini kwamba mmoja wa watuhumiwa hao amekufa kutokana na miripuko hiyo na pia amethibitisha kwamba mtu mmoja amekamatwa katika misako iliofanyika kwenye mji wa kaskazini wa Leeds.Amesema polisi imegunduwa baadhi ya vitu ambavyo vinaweza kuwa mabomu.
Tuhuma kwamba mirupuko hiyo imetelekezwa na washambuliaji wa kujitolea muhanga maisha zimezidi kuongezeka hapo jana baada ya gazeti moja kusema kwamba imetekelezwa na vijana wanne wa Uingereza wenye asili ya Pakistan.
Hata hivyo polisi ya London imejizuwiya kutamka moja kwa moja kwamba miripuko hiyo kwa treni za chini ya ardhi na kwenye basi moja la ghorofa ilikuwa ni kazi ya washambuliaji wa kujitolea muhanga maisha.
Iwapo nadharia ya mauaji ya kujitolea muhanga maisha itathibitika litakuwa ni shambulio la kwanza kabisa la aina hiyo kuwahi kutokea Ulaya ya magharibi.