LONDON: Mkuu wa polisi atetea sera ya kuwauwa watuhumiwa
25 Julai 2005Mkuu wa polisi mjini London,Ian Blair ameeleza masikitiko yake baada ya maafisa wake kumpiga risasi na kumuuwa kwa makosa raia wa Brazil katika kituo cha treni ya chini ya ardhi mjini London siku ya Ijumaa.Kwa wakati huo huo lakini ameitetea sera ya kupiga risasi na kuuwa wale wanaotuhumiwa kuwa washambulizi wa kijitolea muhanga maisha.Imethibitishwa kuwa Jean Charles de Menezes,fundi umeme aliekuwa na umri wa miaka 27 na aliishi London tangu miaka mitatu,hakuwa na kosa na hakuhusika na majeribio ya Alkhamis iliyopita ya kutaka kuripua mabomu mjini London.Waziri wa mambo ya kigeni wa Brazil,Celso Amorim siku ya Jumapili,alikutana na maafisa wa Uingereza mjini London akitaka kupewa maelezo juu ya kitendo cha kupigwa risasi raia wa Brazil.Kwa wakati huo huo ripoti zasema mtu wa tatu amekamatwa kuhusika na jeribio la mashambulio la siku ya Alkhamis mjini London.Mtu huyo amekamatwa kusini mwa London,ambako watu wengine 2 pia walitiwa mbaroni siku ya Ijumaa.Jeribio lililoshindwa,la kutaka kufanya mashambulio siku ya Alkhamis,limetokea majuma mawili baada ya watu 52 kuuawa katika mashambulio ya kujitolea muhanga katika vyombo vya usafiri mjini London.