LONDON: Miripuko minne yatokea leo mjini London, Uingereza
21 Julai 2005Miripuko minne imetokea leo mjini London, Uingereza, wiki mbili baada ya mashambulio ya Julai saba. Milipuko mitatu ilitokea katika vituo vya magarimoshi chini ya ardhi vya Warren Street, Oval na Shepherd´s Bush.
Maofisa wa polisi wamethibitisha kwamba mtu mmoja amejeruhiwa katika mlipuko uliotokea kwenye kituo cha Waren. Abiria waliokuwa katika vituo hivyo wamesema walisikia milio ya risasi, ambayo maofisa wa Scotland Yard wamesema huenda ni sauti zilizosababishwa na milipuko hiyo.
Mlipuko wa nne ulitokea ndani ya basi moja la abiria katika eneo la Hackney. Madirisha ya basi hilo yameharibiwa katika mlipuko huo. Dereva wa basi hilo amesema aliusikia mlipuko huo katika sehemu ya juu ya basi la ghorofa na hakuna abiria aliyejeruhiwa.
Basi hilo nambari 26 lilikuwa likisafiri kutoka Waterloo kwenda Hackney mashariki mwa London. Maeneo ya milipuko hiyo yamefungwa na polisi.