LONDON: Hakuna ushindi bila ya msaada wa Pakistan
30 Septemba 2006Rais Pervez Musharraf wa Pakistan amesema,bila ya msaada wa Pakistan na wa idara yake ya upelelezi,Marekani na washirika wake watashindwa kile kinachoitwa “vita dhidi ya ugaidi”.Musharraf alisema hayo katika mahojiano yake na Radio BBC,baada ya kuulizwa juu ya maoni kuwa Pakistan si mshirika mzuri kupiga vita ugaidi duniani kwa sababu ya uhusiano kati ya ugaidi na nchi yake.Rais Musharraf akaongezea kuwa Pakistan ni mshirika mkuu na ieleweke wazi kabisa kuwa bila ya nchi hiyo na idara ya upelelezi ISI,vita dhidi ya ugaidi havitopata ushindi nchini Afghanistan. Musharraf,kwa mara nyingine tena amekanusha vikali madai yaliotolewa na afisa wa kijeshi wa ngazi ya juu katika idara ya upelelezi wa kigeni ya Uingereza MI6.Ripoti iliyofichuliwa,iliandikwa na afisa huyo baada ya ujumbe wake wa mwezi Juni kutafuta ukweli nchini Pakistan.Musharraf amepokea uhakikisho kutoka waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair kuwa ripoti hiyo haielezi msimamo wa serikali ya Uingereza.