LONDON : Bangladesh na Chad zatopea kwa rushwa
18 Oktoba 2005Kwa mujibu wa uchunguzi wa shirika la kimataifa la Transparency International uliotangazwa leo hii viwango vya kutisha vya rushwa katika sekta ya umma vinaathiri zaidi ya theluthi mbili ya mataifa duniani.
Bangladesh na Chad zinaoongoza kwenye orodha ya kila mwaka ya viwango vya rushwa ya shirika hilo katika nchi 159. Kwa upande wa pili wa mezani Iceland imeonekana kuwa nchi takriban isiokuwa na rushwa.
Peter Eigen mwenyekiti wa Transparency International amesema rushwa miongoni mwa maafisa wa serikali imekuwa ikichochea umaskini katika nchi nyingi zinazoendelea na kwamba tatizo hilo la rushwa lazima lishughulikiwe ipasavyo ili msaada uweze kuleta tija hasa katika kuwakombowa watu na umaskini.
Shirika hilo lenye makao yake mjini Berlin limesema zaidi ya theluthi mbili ya mataifa hayo 159 yalioko kwenye orodha hiyo yamejipatia pointi pungufu ya 5 kati ya 10 na hiyo kuonyesha kuwepo kwa viwango vya juu vya rushwa.
Bangladesh na Chad zote zina pointi 1.7 wakati nchi iliyoonekana haina rushwa Iceland imejipatia pointi 9.7.