LOME: Polisi mjini Lome wawatawanya waandamanaji.
28 Februari 2005Matangazo
Polisi huko Lome iliwabidi kufyatua mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya maelfu ya waandamanaji mjini humo ambao waliutumbukiza mji kwenye taharuki baada ya waandamanaji hao kurusha mawe na kuweka vizuwizi barabarani.
Maandamano hayo yalipangwa na wafuasi wa vyama pinzani nchini Togo siku mbili baada ya Faure Gnassingbe kukubali kung’atuka uongozini.
Lakini waandamanaji wanasema kuwa bado utawala wa Togo unashikiliwa kimabavu.
Wanataka aliyekuwa spika wa bunge wa zamani Fambare Ouattara Natchaba aapishwe kama rais wa mpito wa Togo kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo.
Wanapinga uteuzi wa bwana Abass Bonfoh ambaye ameteuliwa kuwa rais wa mpito siku ya ijumaa baada ya bunge la nchi hiyo kumtangaza kama spika mpya wa bunge la Togo.