Liverpool kumsajili nyota wa Bundesliga Ekitike
21 Julai 2025Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya England walimgeukia Ekitike baada ya Newcastle kukataa kuwauzia mshambuliaji wa Sweden Alexander Isak, ambaye amewekewa bei ya pauni milioni 150 na klabu yake.
Newcastle na Manchester United pia walikuwa wanammezea mate Ekitike ila sasa Liverpool wanaonekana wamewashinda hao mahasimu wao kwa kuipata saini ya nyota huyo.
Inaaminika kwamba Liverpool, wamekubali kulipa pauni milioni 10 zaidi ili kumsajili Mfaransa huyo mwenye miaka 23 ambaye bei yake ya mwisho inaweza kufikia pauni milioni 79.
Ekitike alifunga mabao 22 katika mechi 48 alizoichezea Frankfurt msimu uliopita katika mashindano yote baada ya kujiunga na Frankfurt kutoka PSG.
Liverpool watasafiri na Ekitike kwa ziara yao ya kabla kuanza kwa msimu endapo watakamilisha kwa wakati usajili wake.