M/Kiti wa CHADEMA Tundu Lissu awakosoa viongozi wa Afrika
6 Machi 2025Akiwasilisha mada kwenye kikao cha kujadili masuala ya demokrasia Afrika katika Kitivo cha Sheria kwenye Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, Lissu ameorodhesha njia mbalimbali ambazo viongozi hudai kulinda katiba ilhali huendeleza udhibiti wa kisiasa kwa ajili ya kulinda na kufanikisha maslahi yao binafsi.
Kulingana na Tundu Lissu mada yake ililenga kufafanua jinsi mikakati na mifumo ya uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ilivyoigwa na kuendelezwa na viongozi mbalimbali wa Afrika kung'ang'ania madarakani na pia kudhibiti mifumo yote ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Amelezea kuwa hali hii ambayo imeitumbukiza Afrika katika udikteta huanzia pale viongozi wanapotangulia kwa kuhamasisha hisia na dhana za uzalendo na kuungwa mkono kwa dhati, mara tu baada ya kupata madaraka wao hujenga muundo wa utawala unaokiuka katiba. Ametoa mfano wa serikali ya sasa ya Uganda ambayo imehusisha pakubwa jeshi katika siasa za nchi na kuifanya mojawapo ya taasisi nyeti katika kukuza miundo ya utawala wa kimabavu.
''Kuhusika kwa majeshi katika siasa za taifa ni hatari sana, na Mwalimu Nyerere ndiye aliwafunza viongozi wenzake kuhusisha majeshi na itakuwa vigumu kuondosha hali hiyo.''
Mwenyekiti huyo wa CHADEMA amewataka raia wa Uganda kujua kuwa Rais Yoweri Museveni alikuzwa na kulelewa binafsi na Mwalimu Nyerere na mifumo yote anayotumia kwa sasa kukukandamiza upinzani alijifunza kutoka kwake. Miongoni mwa hadhira ambayo idadi kubwa imekuwa wasomi na wanafunzi wa sheria, washiriki wametoa angalizo kuwa chanzo cha kila utawala kuwakandamiza raia wake ni pale wanaponyimwa uhuru wa kujieleza.
Soma pia:Lissu ambwaga Mbowe uenyekiti CHADEMA
Lakini mmoja kati ya wasomi Dokta Daniel Ruhweza ametoa angalizo kuwa japo hayati Nyerere huenda hakuwahusisha raia katika kufikia maamuzi fulani, lakini baadaye waliona manufaa yake.
''Wakati mwengine kiongozi anafahamu kile tusichoweza kukubaliana nacho ilhali kitakuwa na manufaa kwetu.''
Tundu Lissu ambaye hivi majuzi alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa CHADEMA amehimiza kuwa kama walivyoiga njia za urais wa kipebari kutoka kwa hayati Nyerere, pia waige mfano wake wa kuamua kuachia madaraka kwa hiari na kuanzisha mfumo wa kuwepo kwa awamu za mbili za urais.
''Angalau wajifunze yale mazuri pia hasa ya kuachia madaraka na kuheshimu utawala wa awamu mbili kwa kuchaguliwa.''
Suala lingine ambalo limejadiliwa na washiriki baada ya wasilisho la mwenyekiti Tundu Lissu ni kwamba wanasiasa na wanasheria wana jukumu kubwa kushirikiana katika kuboresha njia za kujenga demokrasia na haki za binadamu kwa kuzingatia kulinda katiba ya nchi.