Lissu akabiliwa na mashitaka ya uhaini baada ya kukamatwa
10 Aprili 2025Lissu amefikishwa mahakamani, baada ya kukamatwa katika ziara yake ya kuhamasisha ajenda ya chama hicho ya Hakuna Mageuzi, Hakuna Uchaguzi. Kabla ya kusomewa shitaka hilo, taarifa ya jeshi la polisi iliyosainiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Marco Chilya, ilieleza kuwa Lissu alikamatwa baada ya kuwepo madai ya kufanya uchochezi na hivyo jeshi hilo linamshikilia kwa mahojiano.
"Jeshi la Polisi limemkamata mwenyekiti huyo wa chadema kufuatia tuhuma zilizokuwa zinapelelezwa za kuhamasisha kutofanyika kwa uchaguzi mkuu," alisema Marco Chilya.
Chadema kumchukulia hatua msemaji wa CCM kutokana na kauli tata
Akizungumzia kukamatwa kwa Lissu na hatua zilizofikiwa kwa sasa, Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa CHADEMA, Gaston Garubindi pamoja na mambo mengine, amehawamasisha wanasheria kujitokeza kumtetea Lissu kwani makosa yake hayana dhamana.
"Tunawaomba mawakili wote kujitokeza, tuwasiliane nao, tufanye logistic kwa ajili ya kumtetea mwenyekiti wa chama ambaye anashitakiwa kwa makosa hayo ya uhaini kwa mujibu wa jeshi la polisi," alisema Gaston Garubindi.
Hata hivyo kesi ya mwenyekiti huyo wa chadema Tundu Lissu, imeahirishwa hadi Aprili 20 na amerejeshwa rumande.
Polisi lilitumia mabomu ya machozi kuwaondoa wafuasi wa CHADEMA
Kando na hayo mkutano wa hadhara uliopangwa kufanyika wilayani Mbinga, ulizuiwa na jeshi la polisi, na mkutano pia wa chama hicho na wanahabari uliopangwa kufanyika kadhalika ulizuiliwa.
Kabla ya Jeshi la Polisi kutoa taarifa hii, sakata la Lissu kukamatwa kumezua mjadala ndani ya bunge la Tanzania na nje ya bunge ambako wadau wamekuwa na maoni tofauti. Mbunge wa Nkasi Kaskazini, CHADEMA Aidan Kenan alizungumza bungeni, huku akilitaka jeshi la polisi litaje sababu za kukamatwa kwa Lissu.
CHADEMA yazinduwa 'Operesheni 255' kudai katiba mpya
Pamoja na kuzuiwa kwa mikutano hiyo na kukamatwa kwa Lissu, kadhalika jeshi la polisi lilitumia mabomu ya machozi kuwaondoa wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wamejikusanya katika eneo la Mfuranyaki ambako mkutano wa Lissu ulipangwa kufanyika. Mchambuzi wa masuala ya siasa na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dokta Richard Mbunda, amesema inawezekana R nne za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania SAMIA Suluhu hassan hazijaeleweka.
"Sasa unapoona kwamba matukio kama haya yanatokea, ambapo nguvu kubwa ya polisi na mabomu yanapigwa unagundua kwamba labda pengine watu wengi hawajaielewa falsafa yake ya kuendesha siasa kwa haki na kwa hoja na kuhakikisha kwamba kila mmoja anazingatiwa katika kutoa maoni yake," Dokta Richard Mbunda.
Muda mchache uliopita CHADEMA kimetoa tamko lake kwa umma likishinikiza jeshi la polisi kumwachia Lissu, jeshi hilo lisijiingize kwenye siasa na wakiwataka wanasheria wote nchini kujitokeza kumtetea mwanasiasa huyo machachari.