LHRC: Watu wasiojulikana wamerejea kwa kasi Tanzania
5 Mei 2025Akisoma maudhui ya ripoti hiyo leo, Mei 5, Kaimu Mkurugenzi wa LHRC, Fulgence Masawe amesema, hali ya haki za binadamu ilizorota kidogo kwa mwaka 2024 ikilinganishwa na mwaka 2023.
Ripoti imebeba dhima isemayo, kurejea kwa watu wasiojulikana ambapo kwa mujibu wa LHRC kumekuwa na ongezeko la mauaji na kupotea kwa watu matukio ambayo LHRC wamesema yanaongezeka hadi wakati ambapo ripoti hiyo inatolewa matukio 63 ya watu kutekwa, kupotea na kuuawa yamebainishwa .
Kadhalika katika ripoti hiyo ilielezwa kuwa, mauaji ya wenza, Imani za kishirikina na matukio 500 ya wananchi kujichukulia sheria mkononi.
Soma pia:Kuongezeka ukandamizaji Yemen kunazorotesha misaada ya kiutu
Sambamba na hayo, haki za kiraia na kisiasa ndizo zilizokiukwa zaidi ikiwamo kuvunjwa kwa haki za binadamu na utawala wa bora wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024.
Matukio ya ukatili kwa wanawake na Watoto nayo ymetajwa kukithiri ambapo asilimia 41 ya Watoto walifanyiwa ukatili na asilimia 29 ya wanawake nao waliathirika na matukio ya ukatili.
Ripoti: Haki katika uchumi binafsi
Pamoja na hayo ripoti hiyo imebainisha kuwa kuna uvunjwaji wa haki za binadamu kutokana na mikopo inayotolewa mitandaoni, hasa katika kipengele cha riba kubwa, kudhalilishwa mitandaoni na kuchukuliwa mali.
ripoti ya LHRC kwa mwaka 2024 imechukua takwimu kutoka mikoa 20 ya Tanzania Bara, kupitia tafiti, ufuatiliaji wa haki, msaada wa kisheria, na uchambuzi wa taarifa za vyombo vya habari.
Soma pia:Dunia yaadhimisha siku ya watu waliopotea na waliotoweka
Kadhalika ripoti hiyo imetoa mapendekezo kadhaa kwa serikali ikiwamo kutoa taarifa kuhusu matukio ya utekwaji, kushambuliwa na kupotea kwa watu, kusimamia haki za wananwake na Watoto na watu wenye ulemavu Tanzania.