Leseni bandia: Vituo vya afya 158 vyafungwa Kenya
9 Septemba 2025Operesheni hiyo ya ukaguzi ilihusisha vituo 288, ambapo vingine 25 vilishushiwa hadhi na 105 vikiruhusiwa kuendelea kufanya kazi katika kiwango chao cha sasa. Afisa Mtendaji Mkuu wa KMPDC, Dkt. David Kariuki, amesema vituo vingi vilivyofungwa havikuwa vimesajiliwa, vilikuwa na wahudumu wasio na sifa zinazohitajika, au vilikuwa vikiendeshwa bila kuzingatia viwango vilivyowekwa, hali iliyokuwa tishio kwa usalama wa umma.
Msako huo unatekelezwa kwa ushirikiano na serikali za kaunti na wadhibiti wengine wa afya chini ya Kanuni za Ukaguzi na Utoaji Leseni za mwaka 2022. Dkt. Kariuki aliongeza kuwa baadhi ya vituo hivyo havikuwa na miundombinu muhimukama vile duka la madawa, wodi za wazazi au hata maabara, huku vingine vikifanya kazi kwenye mazingira duni ya usafi na mifumo mibovu ya utupaji taka inayoweza kuhatarisha maisha ya wagonjwa.
"Tulitambua hitilafu zilizokuwepo na tukazitaja, lakini tuliwafahamisha kuwa wanastahili kuzingatia utaratibu uliopo, wasitishe kuendesha kazi hospitalini hadi uchunguzi ukamilike.”
Hatua inakusudiwa kuendeleza uwajibikaji na uboreshaji wa huduma za afya
Baraza hilo lilibainisha kuwa ingawa ukaguzi ni wa kawaida, zoezi hilo limekuwa likifanyika mara kwa mara kufuatia ongezeko la visa vya udanganyifu na unyonyaji wa wagonjwa. Taarifa kuhusu vituo vilivyofungwa pia imeshirikishwa na serikali za kaunti, Mamlaka ya Afya ya Jamii na wadhibiti wengine, ili kuhakikisha utekelezaji wa sheria.
Dokta Kariuki amesema kuwa kanuni hizi hazikusudiwi tu kudhibiti utaratibu, bali pia kuendeleza uwajibikaji, uwazi na uboreshaji endelevu wa huduma za afya. Afisa huyo alisisitiza kuwa ni vituo vilivyosajiliwa na kupewa leseni na Baraza la Madaktari pekee ndivyo vinavyoruhusiwa kisheria kufanya kazi.
Ili kuwaongoza wananchi, KMPDC imesema itachapisha majina ya vituo vilivyofungwana ikawahimiza Wakenya kuthibitisha hadhi ya usajili wa hospitali na wahudumu wa afya kabla ya kutafuta huduma. Hayo yajiri wakati Rais William Ruto akisisitiza kwamba wote waliohusishwa kwenye kashfa ya Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) watachukuliwa hatua kali za sheria.
"Ule wizi uliangusha mpango wa NHIF, mpaka kukawa na madeni ya shilingi bilioni 30, haiwezi kufanyika ndani ya SHA. Bado kuna hospitali kwenye kaunti ambazo zinaitisha pesa wananchi, nyinyi mnanielewa.”
Hospitali 1000 kote nchini zimepatikana kwenye kashfa hiyo ya SHA, huku shilingi bilioni 24 zikihofiwa kutoweka. Wakenya sasa wanamshinikiza Waziri wa Afya Adan Duale kuwajibika kwa kuondoka afisini kutokana na kashfa hiyo.