Leo XIV aongoza misa ya kwanza kama papa
9 Mei 2025Matangazo
Kiongozi mpya wa kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV, leo ameongoza ibada ya kwanza ya misa, siku moja baada ya kuwa Mmarekani wa kwanza kuliongoza kanisa hilo.
Mzaliwa huyo wa Chicago Robert Francis Prevost alichaguliwa jana Alhamisi kuwa papa wa 267, kiongozi wa kiroho wa waumini bilioni 1.4 wa kanisa Katoliki, kufuatia mkutano maalumu wa makadinali wenzake katika makazi rasmi ya papa kanisa la Sistine mjini Vatican.
Papa huyo mwenye umri wa miaka 69, amerejea katika kanisa hilo kuongoza misa ya faragha na makadilani iliyooneshwa moja kwa moja na makao makuu Vatican, akitoa hotuba yake ya kwanza kama papa iliyosubiriwa sana kwa hamu.