Lengo la shambulio la treni Ujerumani bado halijajulikana
4 Julai 2025Kulingana na aliyeshuhudia tukio hilo, raia huyo wa Syria anaedaiwa kuwajeruhi abiria kadhaa waliokuwa katika treni ya mwendo kasi nchini Ujerumani iliyotoka Hamburg kuelekea katika mji mkuu wa Austria Vienna, alisali kabla ya shambulio hilo.
Mwendesha mashitaka Thomas Rauscher, alisema mshukiwa huyo aliye na umri wa miaka 20 alisikika akisema "Allahu Akbar," yaani Mungu ni mkubwa pamoja na maneno mengine ya kiarabu. Hata hivyo haijakuwa wazi kama tukio hilo la jana 03.07.2025 lilikuwa na lengo lolote la kigaidi.
Aliyewashambulia watu kwa kisu Ujerumani ahukumiwa miaka 14 jela
Watu watano walijeruhiwa akiwemo mshukiwa mwenyewe, baada ya kutoa shoka alilokuwa amelibeba ndani ya treni hiyo ya mwendo kasi iliyokuwa inapitia jimbo la Kusini mwa Ujerumani la Bavaria na kuwashambulia abiria wanne, ambao ni raia wenzake wa Syria walio na miaka 15, 24, na 51 pamoja na raia mmoja Mjerumani aliye na umri wa miaka 38.
Mwendesha mashitaka Rauscher amesema mshukiwa huyo anachunguzwa juu ya jaribio la mauaji katika kesi ya kijana wa miaka 24 na 38 na pia kuchunguzwa kwa kuwasababishia madhara makubwa ya kimwili abiria wengine wawili.
Mshukiwa alipelekwa hospitali baada ya tukio hilo na damu yake ilipatikana kuwa na chembe chembe za madawa ya kulevya.
Ulaya kuweka masharti zaidi katika sera zake za uhamiaji
Wakati huo huo, waziri wa ndani wa Ujerumani Alexander Dobrindt anatarajiwa kuwaalika wenzake kutoka nchi jirani kwa mazungumzo ya kuweka masharti zaidi katika sera za Ulaya kuhusu uhamiaji. Mkutano huo unatarajiwa kufanyika maeneo ya milima ya Bavaria manmo Julai 18.
Msemaji wa wizara hiyo amesema mkutano huo unatarajiwa kutoa majibu ya pamoja kuhusu sera hiyo ya uhamiaji. Kando na mawaziri wa ndani wa Ufaransa, Poland, Austria, Denmark na Jamhuri ya Czech, Kamishna wa mambo ya ndani na uhamiaji wa Umoja wa Ulaya Magnus Brunner, pia atashiriki mkutano huo.
Ujerumani inapigia tena kura mageuzi katika sheria ya uhamiaji
Mawaziri hao pia watajadili hatua za kukabiliana na biashara ya usafirishaji haramu wa watu pamoja na njia za kuwarejesha watu makwao. Nchi wanachama za Umoja wa Ulaya zimekuwa zikijadili namna ya kuweka hatua kali zaidi chini ya mfumo wa kuomba hifadhi wa Umoja huo unaojulikana kama GEAS utakaoanza kufanya kazi kuanzia mwaka 2026.
Chini ya mageuzi ya sasa, nchi wanachama haziruhusiwi kuwapeleka wanaotafuta hifadhi kwa nchi zilizo nje ya Umoja huo, ikiwa muomba hifadhi hana mafunganamo yoyote na nchi hiyo. Hata hivyo, nchi nyingi zinataka kipengele hicho cha mageuzi kifutiliwe mbali.