Lavrov: Putin yuko tayari kukutana na Zelenskiy kwa masharti
21 Agosti 2025Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov, amesema Rais Vladimir Putin yuko tayari kukutana na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, lakini ni baada ya masharti kadhaa kutimizwa. Kauli hii imeibua mjadala mpya kuhusu mustakabali wa juhudi za kidiplomasia za kumaliza vita vilivyoendelea kwa zaidi ya miaka mitatu.
Lavrov alieleza kuwa kabla ya kikao cha ana kwa ana kufanyika, masuala yote muhimu lazima yashughulikiwe ipasavyo, ikiwa ni pamoja na mashauriano ya kina yanayoendeshwa na wataalamu na mawaziri wa pande zote mbili. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa makubaliano yoyote yajayo yatakuwa na msingi wa kitaalamu na kisiasa thabiti.
"Rais wetu amesisitiza mara kadhaa kuwa yuko tayari kukutana, akiwemo na Bw. Zelenskyy, kwa sharti kwamba masuala yote yanayohitaji kujadiliwa katika ngazi ya juu yatafanyiwa kazi ipasavyo, na wataalamu pamoja na mawaziri wataandaa mapendekezo sahihi. Na bila shaka, pale na iwapo — na ninatumai itakuwa pale — itakapofika wakati wa kusaini makubaliano ya baadaye, suala la uhalali wa mtu atakayesaini makubaliano hayo kwa upande wa Ukraine litakuwa limepatiwa ufumbuzi,” alisema Lavrov siku ya Alhamisi.
Miongoni mwa masharti hayo ni mjadala kuhusu uhalali wa Rais Zelenskyy, baada ya uchaguzi wa Ukraine kuahirishwa kutokana na hali ya vita. Moscow imesema haiwezi kusaini makubaliano yoyote bila ufafanuzi wa kisheria kuhusu nafasi ya Zelenskyy kama kiongozi halali wa Ukraine.
Mashauriano makubwa kuhusu dhamana na usalama
Kwa upande wa Kyiv, Rais Zelenskiy amesema mashauriano makubwa yanaendelea na washirika wa kimataifa ili kufafanua aina ya dhamana za usalama ambazo Ukraine inaweza kupata. Amesema matokeo ya mashauriano hayo yanatarajiwa kujulikana ndani ya siku kumi zijazo, hatua ambayo inaweza kufungua njia kwa mazungumzo ya ana kwa ana na Putin.
Zelenskyy pia hakufuta uwezekano wa kikao cha pande tatu kitakachoshirikisha pia Rais wa Marekani Donald Trump. Tayari mataifa kadhaa, yakiwemo Uswisi, Austria na Uturuki, yametajwa kama maeneo yanayoweza kuwa wenyeji wa mkutano huo wa kihistoria.
Wakati mashauriano haya yakiendelea, uhasama kwenye uwanja wa vita unaongezeka. Jeshi la anga la Ukraine limesema Urusi imetekeleza moja ya mashambulizi makubwa zaidi mwaka huu, ikirusha droni 574 na makombora 40 ya masafa marefu.Mashambulizi hayo yameharibu miundombinu muhimu na kuua raia, ikiwa ni pamoja na mlipuko ulioharibu majengo 26 na shule ya awali mjini Lviv.
Urusi imesema mashambulizi hayo yalilenga maeneo ya viwanda vya kijeshi na maghala ya silaha, huku ikikanusha madai ya kushambulia maeneo ya raia. Hata hivyo, maafisa wa Ukraine wamekosoa vikali mashambulizi hayo, wakisema Moscow "haitafuti amani” na badala yake inaendelea kutumia nguvu ili kuongeza shinikizo katika mazungumzo.
Wakati huo huo, Rais Trump ameongeza kasi ya juhudi za kidiplomasia. Baada ya kikao chake na Putin huko Alaska wiki iliyopita, alikutana na Zelenskyy na viongozi wa Ulaya Ikulu ya White House mapema wiki hii. Lengo kuu la mashauriano haya ni kusaka suluhu ya kudumu inayoweza kumaliza vita bila kulazimisha Ukraine kutoa sehemu kubwa ya ardhi yake.
Nchi za Ulaya, kwa upande mwingine, zimekuwa zikiweka shinikizo kwa Moscow ili kuonyesha nia ya kweli ya kusitisha mapigano. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johann Wadephul, ameitaka China kutumia ushawishi wake kumshinikiza Putin kukubali kusitishwa kwa vita, akisema Beijing inaweza kuwa mshirika muhimu iwapo itaamua kushiriki kikamilifu katika juhudi za amani.
Licha ya kuongezeka kwa juhudi za kidiplomasia, changamoto bado ni kubwa. Mashambulizi ya makombora na droni yameendelea, huku Ukraine nayo ikiendeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi ndani ya Urusi kwa kutumia droni zake za masafa marefu, zikilenga miundombinu ya mafuta na nishati.
Kwa wachambuzi wa masuala ya kimataifa, hali hii inaonyesha kuwa ingawa kuna mwanga wa matumaini ya majadiliano, njia ya kufikia makubaliano ya kudumu bado ni ndefu na yenye vizuizi vingi — vikubwa zaidi vikiwa ni masharti ya kisiasa na kijeshi yanayowekwa na pande zote mbili.