Lammy kuwa mwenyeji wa Weimar+ kwa ajili ya Ukraine
12 Mei 2025Lengo la kundi la Weimar+ ni kuhakikisha Ulaya inakuwa na sauti moja katika masuala ya usalama wa kikanda na kijiografia.
Mkutano huo utajadili kando na mambo mengine, msaada kwa Ukraine na ushirikiano mkubwa wa ulinzi wa kikanda kabla ya kufanyika mkutano mwengine wa Waziri Mkuu Keir Starmer na viongozi wa Umoja wa Ulaya wiki ijayo.
Kwa mujibu wa maafisa wa wizara hiyo ya mambo ya nje ya Uingereza, Lammy anapanga kutangaza vikwazo zaidi dhidi ya Urusi, siku chache tu baada ya viongozi wa Ulaya kuonya kuchukua hatua zaidi iwapo Urusi haitaonyesha ushirikiano katika kupatikana amani nchini Ukraine.
Soma pia: Viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Uingereza na Poland ziarani nchini Ukraine
Mkutano huo unafanyika baada ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kueleza utayari wa kufanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin nchini Uturuki, baada ya kiongozi huyo wa Urusi kusema kuwa anataka kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na serikali mjini Kiev.
Miito imetolewa kwa Urusi kuukubali mpango wa kusitisha mapigano kwa siku 30, ambao Ukraine inataka uanze kutekelezwa kuanzia leo Jumatatu.