FC Köln yarejea ligi kuu ya Bundesliga
19 Mei 2025Katika mchezo wa mwisho wa msimu, Köln ilifunga mabao mawili katika dakika 29 za mwanzo kupitia kwa Eric Martel na Luca Waldschmidt.
Florian Kainz aliongeza la tatu katika dakika ya 76, na mchezaji anayestaafu, Mark Uth, alifunga la nne dakika tatu kabla ya kipenga cha mwisho. Hii ilihakikisha kupanda kwao Bundesliga pamoja na Hamburg SV, ambao walimaliza na pointi 59, mbili nyuma ya Köln.
Elversberg, waliomaliza katika nafasi ya tatu, watacheza mechi ya mchujo ili kutafuta tiketi ya kupanda daraja dhidi ya Heidenheim, waliomaliza katika nafasi ya 16 katika jedwali la Bundesliga.
Funkel: Kocha wa Muda Atafakari Kuendelea
Friedhelm Funkel, mwenye umri wa miaka 71, alichukua jukumu la ukocha wa muda baada ya kutimuliwa kwa Gerhard Struber na Christian Keller. Aliiongoza timu kushinda michezo miwili ya mwisho ya msimu dhidi ya Nürnberg na Kaiserslautern, na hivyo kuhakikisha kupanda daraja kwa Bundesliga. Funkel, ambaye ana rekodi ya kuwa na mafanikio mengi ya kupanda daraja kuliko makocha wengine, alisema: "Niko wazi kwa kila kitu, ikiwa ni pamoja na kuendelea na kazi hii." Aliongeza kuwa anapenda klabu hii na amefurahi sana kufanya kazi nayo tena.
Baada ya kuachana na Fortuna Düsseldorf miaka mitano iliyopita, Funkel alitangaza kuwa hatofundisha tena klabu nyingine. Hata hivyo, ameweza kurudi Köln mara mbili na pia alichukua jukumu la ukocha wa Kaiserslautern msimu uliopita.
Maamuzi kuhusu mustakabali wake kama kocha wa kudumu wa Köln yatategemea majadiliano na uongozi wa klabu. FC Cologne