Kwanini Waafrika husafiri nje kusaka matibabu?
5 Agosti 2025Chini ya Azimio la Abuja la mwaka 2001, nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) zilikubaliana kukomesha mgogoro wa ufadhili wa huduma za afya barani kwa kuahidi kutenga asilimia 15 ya bajeti zao za kila mwaka kwa huduma za afya. Lakini zaidi ya miaka ishirini baadaye, ni nchi tatu tu — Rwanda, Botswana na Cape Verde — ambazo zimekuwa zikitimiza au kuzidi kiwango hicho kwa uthabiti.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linaripoti kuwa zaidi ya nchi 30 wanachama wa Umoja wa Afrika hutenga chini ya asilimia 10 ya bajeti zao kwa huduma za afya, huku baadhi zikitenga kati ya asilimia 5 hadi 7 pekee.
Jamila Atiku, mtafiti wa afya ya umma nchini Nigeria, aliambia DW kwamba "Nigeria imekuwa ikitenga kati ya asilimia 4 hadi 6 ya bajeti ya kila mwaka kwenye sekta ya afya," akisisitiza kuwa wanasiasa hujali zaidi kuhusu miradi mingine ya maendeleo kama barabara, ilhali madaktari na wataalamu wa afya wamekuwa wakigoma mara kwa mara kwa sababu ya malipo duni.
Ingawa uamuzi wa ni wapi kutafuta matibabu ni wa kibinafsi sana, matukio ya mara kwa mara ambapo viongozi wa Afrika wamekuwa wakitafuta matibabu nje ya nchi yameweka wazi tatizo la uwekezaji mdogo katika huduma za afya za ndani.
Vifo vya viongozi wa zamani Muhammadu Buhari wa Nigeria na Edgar Lungu wa Zambia katika vituo vya matibabu vya nje ya nchi havijatuliza tuhuma kwamba viongozi wa Afrika wamepuuza mifumo ya afya ya umma katika mataifa yao.
Kwa kiwango kikubwa, viongozi wanawajibika kwa maendeleo ya huduma bora za afya kwa raia wa nchi zao.
Uwekezaji duni kwenye huduma bingwa za matibabu watajwa
Hata hivyo, ukosefu wa huduma za kitaalamu, vifaa duni katika hospitali, na hofu za kiusalama kwa wanasiasa ni baadhi ya sababu zinazochochea "utalii wa matibabu.”
Sababu nyingine, kulingana na mtetezi wa haki za afya kutoka Zimbabwe, Chamunorwa Mashoko, ni utegemezi mkubwa kwa misaada ya kigeni.
"Kati ya nchi 54 za Afrika, zaidi ya nchi 32 hazitengi bajeti kubwa kwa afya, hali inayochangiwa na utegemezi wa misaada ya wafadhili," aliiambia DW.
Mashoko anasema Afrika inashindwa kutambua kwamba ufadhili wa kigeni katika afya ni sehemu ya diplomasia tu na haushughulikii changamoto halisi za kiafya.
Nchi za Afrika hupokea zaidi ya dola bilioni 60 kama misaada ya sekta ya afya, kiwango ambacho ni sehemu ndogo sana ya mahitaji halisi ya kifedha ya bara hilo kwa huduma za afya.
Huduma ambazo mara nyingi hutafutwa nje ya nchi ni pamoja na matibabu ya saratani, moyo, neva, mifupa, upandikizaji wa viungo, uzazi wa kusaidiwa, na huduma za watoto kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya kurithi ambayo ni nadra.
Zaidi ya Waafrika 300,000 husafiri kila mwaka kwenda India kwa ajili ya matibabu, wakitumia zaidi ya dola bilioni 2 kwa mwaka.
Makadirio yanaonesha kuwa India inaweza kupata hadi dola bilioni 13 kupitia "utalii wa matibabu” kufikia mwaka 2026 chini ya mpango wao wa "Heal in India”.