Kwa nini Ulaya Kusini inaongoza ukuaji wa ukanda wa euro?
14 Februari 2025Miaka michache tu iliyopita, Ureno, Italia, Uhispania, na Ugiriki zilichukuliwa kama watoto wenye matatizo ndani ya Jumuiya ya Ulaya (EU), hasa kati ya nchi 20 zinazounda ukanda wa euro.
Hali hii imebadilika kabisa, huku Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez, akisisitiza hivi karibuni kwenye Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) huko Davos kwamba nchi za kusini mwa Umoja wa Ulaya zinaweza pia "kutoa suluhisho kwa matatizo ya pamoja."
Zaidi ya muongo mmoja tangu mgogoro wa madeni barani Ulaya ulipozipeleka nchi hizi nne karibu na kuporomoka kifedha, ukuaji imara wa uchumi umerudi katika eneo la kusini mwa bara hilo.
Kwa mfano, Uhispania imekuwa mzalishaji na msafirishaji mkubwa wa nishati jadidifu — hasa nguvu za jua — jambo linaloinufaisha yenyewe na nchi nyingine katikati ya mgogoro wa nishati uliosababishwa na vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.
Mgawanyiko mpya wa kaskazini na kusini katika EU
Katika mtazamo mpana wa Ulaya, hali ya uchumi bado si nzuri. Uchumi wa ukanda wa euro umekwama bila ukuaji. Katika robo ya nne ya mwaka 2024, uchumi wa ukanda huo haukukua ikilinganishwa na robo iliyopita. Kwa ujumla, robo ya kiangazi pekee ndiyo ilionyesha mwelekeo mzuri kidogo, ambapo pato la taifa (GDP) liliongezeka kwa asilimia 0.4 kwa mwaka.
Wataalamu wengi wanaelekeza lawama kwa udhaifu wa kiuchumi unaoendelea katika nchi kubwa zaidi kiuchumi barani Ulaya, Ujerumani, kama sababu kuu ya hali hii.
GDP ya Ujerumani ilipungua kwa asilimia 0.2 katika robo ya nne na pia kwa mwaka mzima wa 2024. Alexander Krüger, mchumi mkuu katika moja ya benki kubwa zaidi ya binafsi nchini Ujerumani, Hauck Aufhäuser Lampe Privatbank, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba Ujerumani "inaendelea kusalia nyuma" ndani ya ukanda wa euro na hata kimataifa.
Hakuna nguvu ya kutosa kuendesha uchumi mzima
Wakati uchumi wa nchi kubwa zaidi katika ukanda wa euro ukiwa katika hali ngumu, je, mataifa ya kusini mwa Ulaya yanaweza kuwa injini mpya ya ukuaji wa Umoja wa Ulaya?
Mchumi Gabriel Felbermayr anaamini kuwa hayawezi kwa sababu "kiuchumi, bado ni madogo sana."
Mkurugenzi huyo wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi ya Austria (WIFO) aliiambia DW kwamba Ujerumani na Ufaransa pekee zinachangia zaidi ya asilimia 50 ya pato la ukanda wa euro.
Aidha, Austria, Slovenia, Slovakia, na Uholanzi zinapaswa pia kuzingatiwa kama sehemu ya "kanda imara ya viwanda ya kaskazini" ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto kubwa.
Aliongeza kuwa nchi za EU ambazo haziko kwenye ukanda wa euro, hasa Jamhuri ya Czech na Poland, pia kwa kiwango fulani "zinaathirika na udhaifu wa sekta ya viwanda ya EU."
Bei za nishati ni muhimu kwa ukuaji wa ukanda wa euro
Kwa hiyo, kwa nini uchumi wa kusini mwa Ulaya unafanya vizuri, ilhali nchi zilizo na nguvu za jadi za kiuchumi zinaendelea kupambana?
Hans-Werner Sinn, mmoja wa wachumi mashuhuri wa Ujerumani na aliyekuwa mkuu wa taasisi ya utafiti wa kiuchumi Ifo, anaona kuwa kuna sababu za nje na maamuzi ya kisiasa yanayochangia hali hii.
"Ujerumani imeathirika sana katika miaka ya hivi karibuni kutokana na mgogoro wa nishati, ambao ulisababishwa na mchanganyiko wa vita vya Ukraine na uhaba wa nishati uliosababishwa na sera za ndani," alisema katika mahojiano na DW.
Soma zaidi: Waziri Mkuu wa Hungary afanya mazungumzo na Rais wa Urusi Vladmir Putin
Anakosoa juhudi za kuhama kutoka nishati ya kisukuku kwenda nishati jadidifu, akidai kuwa "EU na Ujerumani zimepoteza uwiano", hali iliyosababisha Ujerumani kulipa "bei ya juu zaidi ya umeme duniani kwa sasa."
Sinn alieleza kuwa hii imeathiri sana sekta ya kemikali na pia sekta ya magari ya Ujerumani. "Kanuni za matumizi ya mafuta kwa magari katika Umoja wa Ulaya zimeharibu ushindani wa sekta ya magari."
Felbermayr anakubaliana na maoni ya Sinn, akisema kuwa sekta kuu za kiuchumi katika nchi za kusini mwa EU, kama vile utalii na kilimo, "hazihitaji mchango mkubwa wa viwanda katika thamani ya jumla ya uchumi."
Hii ina maana kwamba gharama kubwa za nishati, vita vya kibiashara, na changamoto za upunguzaji wa uzalishaji wa kaboni zinaziathiri zaidi nchi za kaskazini mwa Ulaya kuliko zile za kusini.
Felbermayr pia alibainisha kuwa viwango vya mfumuko wa bei katika nchi za kusini mwa EU vimekuwa vya chini kuliko katika nchi za kaskazini tangu mwaka 2010, hali iliyozifanya ziwe na ushindani mkubwa zaidi.
Soma pia: Viongozi wa Ulaya wahimiza mageuzi ya kiuchumi ya kanda hiyo
"Juhudi za mageuzi baada ya mgogoro wa madeni wa ukanda wa euro zimeleta matokeo chanya — hasa kwa Ugiriki, Uhispania, na Ureno," aliongeza.
Vikwazo vya biashara vya Trump vyatishia uchumi wa ukanda wa euro
Jörg Krämer, mchumi mkuu wa benki ya Ujerumani, Commerzbank, anaamini kuwa hakuna matumaini makubwa ya uchumi wa ukanda wa euro kuimarika haraka na anatarajia "urejeo hafifu kwa kiwango cha juu zaidi." Akizungumza na shirika la habari Reuters, alisema kuwa "mgogoro mkubwa wa kimuundo katika sekta ya viwanda na vitisho vya ushuru kutoka kwa Trump vinaathiri kila kitu."
Rais wa Marekani, Donald Trump, ametishia kuiwekea Ulaya ushuru wa juu zaidi, jambo ambalo litaiathiri sana Ujerumani, ambayo uchumi wake unategemea sana mauzo ya nje.
Sebastian Dullien, mkurugenzi wa utafiti katika Taasisi ya Sera ya Uchumi Mpana (IMK) ya Hans-Böckler Foundation nchini Ujerumani, pia haoni dalili za uchumi kuimarika. Alisema kuwa kuna sababu kadhaa zinazochangia mdororo wa uchumi wa muda mrefu wa Ujerumani.
Kati ya hizo, muhimu zaidi ni sera za viwanda za China zinazoshindana kwa ukali, ambazo zinaathiri mauzo ya nje ya Ujerumani, pamoja na viwango vya juu vya riba vya Benki Kuu ya Ulaya (ECB), vinavyopunguza uwekezaji.
Akizungumza katika Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) huko Davos hivi karibuni, Waziri wa Uchumi na Mazingira wa Ujerumani, Robert Habeck, alionekana hatimaye kukubali ukubwa wa changamoto za kiuchumi za nchi yake, akisema kwamba Ujerumani "imepuuza kwa kiasi fulani ukweli kwamba huu si mgogoro wa muda mfupi tu, bali ni wa kimuundo."
Soma pia: Scholz azuru Kazakhstan kuimarisha biashara, ugavi wa mafuta
Aliongeza kuwa changamoto hizi zinaonekana zaidi katika sekta ya viwanda, ambayo inakabiliwa na gharama kubwa za umeme. Alikiri kuwa biashara ya nje ya Ujerumani inazidi kudhoofika, hali ya kujiamini kwa walaji inapungua, na akasisitiza kuwa 'tunapaswa kubuni upya mtindo wetu wa biashara.'
Njia ya kusonga mbele
Licha ya changamoto za kiuchumi za sasa, Tume ya Ulaya ina matumaini kwamba urejeo wa uchumi utaanza kuonekana mwaka 2025, na hata inatarajia uchumi wa ukanda wa euro kukua kwa asilimia 1.3. Benki Kuu ya Ulaya (ECB), ambayo ilipunguza viwango vya riba kutoka asilimia 3 hadi 2.75 wiki iliyopita, inatarajiwa kuendelea kushusha viwango hivyo kwa mwaka mzima.
Kuhusu tofauti za ukuaji kati ya kaskazini na kusini mwa ukanda wa euro, mkuu wa WIFO, Gabriel Felbermayr, anaona kuwa hii si jambo la ajabu. "Wakati mwingine, kaskazini yenye nguvu ya viwanda inaongoza, na wakati mwingine kusini inayotegemea huduma inashika nafasi ya juu. Hali hii si tofauti na ilivyo katika uchumi mkubwa kama Marekani."
Amebainisha kuwa jambo la muhimu kwa sasa ni kwa nchi za kaskazini "kusukuma mbele mageuzi muhimu ili kuongeza ushindani wao, huku zile za kusini zikiendelea na juhudi zao za uimarishaji wa uchumi."
Kwa kufanya hivyo, soko la pamoja la Ulaya litaimarika na kuwa "mfumo wa kusawazisha tofauti za kiuchumi kati ya maeneo mbalimbali ndani ya EU."