Kwa nini Marekani inataka kuiadhibu Afrika Kusini?
11 Februari 2025Utawala wa Trump umesema kuwa sheria ya umiliki wa ardhi ya Afrika Kusini iliyopitishwa hivi karibuni ni ubaguzi wa "wazi" dhidi ya jamii ya wazungu ambao wana asili ya Uholanzi na nchi nyingine za kikoloni za Ulaya.
Utawala huo wa Trump umetamka wazi kwamba serikali ya Pretoria imeruhusu mashambulizi ya vurugu dhidi ya jamii za makaburu. Aidha pia utawala wa Trump umeishutumu Afrika Kusini kwa kuunga mkono "pande mbaya" duniani ikiwemo kundi la wanamgambo wa Kipalestina wa Hamas, Urusi na Iran.
Soma: Ramaphosa asema yupo tayari kuzungumza na Rrump kuhusu usitishaji misaada
Ugawaji ardhi nchini Afrika Kusini umekuwa ni suala tete na lenye kuzusha hisia zinazohusiana na ubaguzi wa rangi kwa zaidi ya miaka 30 tangu kukomeshwa kwa mfumo wa kibaguzi chini ya utawala wa wazungu wachache mwaka 1994.
Suala hilo lilipatwa kumulikwa tena kimataifa baada ya Trump na mshauri wake mzaliwa wa Afrika kusini Elon Musk kukosoa sera za serikali ya Pretoria kuwa zenye kuwabagua makaburu, wakati mwingine kwa kauli za uongo.
Ni sheria gani ambayo Trump anaizungumzia?
Sheria mpya ya kusimamia umiliki wa ardhi inaipatia serikali ya Afrika Kusini wigo mpana wa kutaifisha ardhi kutoka kwa watu binafsi endapo tu itakuwa ni kwa maslahi ya umma na chini ya masharti fulani.
Trump alieleza kwamba serikali ya Afrika Kusini inafanya "makosa makubwa" na kudai kwamba ardhi imekuwa ikichukuliwa kutoka kwa "watu wa hadhi fulani".
Hata hivyo kulingana na makundi yanayoipinga sheria hiyo nchini Afrika Kusini, hakuna ardhi ambayo imenyakuliwa. Serikali ya Afrika Kusini inasema haki za mali za watu binafsi zinalindwa na kwamba maelezo ya Trump kuhusiana na sheria hiyo yana taarifa za uongo na upotoshaji.
Hata hivyo, sheria hiyo imezusha wasiwasi nchini humo, hususan kwa makundi yanayowakilisha sehemu ya jamii za wazungu, ambao wanasema bila shaka watalengwa chini ya sheria hiyo na ardhi yao.
Chini ya mfumo wa kibaguzi wa rangi, ardhi ya watu weusi iliporwa na wakalazimishwa kuishi katika maeneo yaliyotengwa mbali na wazungu.
Hivi sasa wazungu ni asilimia 7 ya idadi ya wakazi wa Afrika Kusini wapatao milioni 62 lakini wanamiliki asilimia 70 ya mashamba binafsi na serikali inasema ukosefu huo wa usawa unapaswa kushughulikiwa.
Makaburu ni akina nani?
Makaburu ama wakijulikana kama Afrikaana ni kundi la wazungu wa Afrika Kusini ambao ni walowezi wa Kiholonzi waliowasili miaka karibu 370 iliyopita. Wanazungumza kiafrikaana, mojawapo ya lugha 11 rasmi za nchi hiyo na wanaunda jamii kubwa ya wakulima wa vijijini nchini Afrika Kusini.Marekani yaiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC
Makaburu walikuwa kiini cha utawala kibaguzi na mivutano baina yao na vyama vya kisiasa vya weusi ilidumu baada ya ubaguzi wa rangi, ingawa nchi hiyo ilifanikiwa katika suala la maridhiano ya jamii tofauti huku makaburu wakijiona kuwa sehemu ya Afrika Kusini. Trump anasema kwamba ataanzisha mpango wa kuwapatia hifadhi wakulima wa kizungu wa Afrika Kusini na familia zao kama wakimbizi.
Elon Musk anahusikaje?
Bilionea huyo mmiliki wa Tesla na mshirika wa Trump alizaliwa na kukulia Afrika Kusini lakini aliondoka alipomaliza sekondari mwishoni mwa miaka ya 80 wakati nchi hiyo ilipokuwa chini ya utawala wa kibaguzi. Kwa miaka mingi ameukosoa utawala wa sasa akiushutumu kwa sera dhidi ya wazungu, kutojali na hata kuhimiza "mauaji ya halaiki" kwa baadhi ya wakulima wa kizungu.
Musk pia ameishutumu Afrika Kusini kwa kuwa na sheria za kibaguzi za umiliki baada ya kushindwa kupata kibali cha huduma yake ya mtandao wa Starlink kwa kutotimiza vigezo.Rais Trump asaini amri kuidhinisha vikwazo dhidi ya ICC
Amri ya Trump inaagiza nini?
Amri ya Trump inasimamisha mamilioni ya dola yanayotolewa kila mwaka na Marekani kwa Afrika Kusini, haswa kusaidia mapambano ya HIV/AIDS. Marekani iliipatia Afrika Kusini kiasi cha dola milioni 440 mwaka jana na inatoa asilimia 17 ya ufadhili katika mpango wa HIV kupitia mpango wa ofisi ya rais.
Nchi hiyo ina karibu watu milioni 8 wenye maambukizi ya HIV huku milioni 5.5 wakipatiwa matibabu ya kupunguza makali na ufadhili wa Washington umekuwa na umuhimu katika kuendesha miradi ya kitaifa ya HIV.