Kwa nini Ethiopia na Eritrea ziko ukingoni kuingia vitani?
14 Machi 2025Hofu ya mgogoro mpya inahusishwa na mgawanyiko uliopo kwenye kundi la TPLF, kutokana na mvutano ulioanza tangu mwishoni mwa mwaka uliopita. Kundi lililojitenga ndio sasa linasimamia eneo la Tigray kwa baraka za serikali kuu ya Ethiopia huku upande uliobakia ukipinga hatua hiyo.
Serikali kuu ilimteua mwanasiasa mkongwe wa Tigray, Getachew Reda, kama mkuu wa utawala wa mpito katika mkoa wa Tigray. Na wiki ilyopita aliwasimamisha kazi majenerali watatu katika Kikosi cha Ulinzi cha Tigray, akilishutumu kundi la upinzani kwa kujaribu kulichukua eneo lote la Tigray. Utawala wa mpito unawatuhumu wapinzani kwa kushirikiana na Eritrea.
Soma pia: Abiy Ahmed asema nchi yake haitoingia vitani na majirani
Lakini anapingwa vikali na mshirika wake wa zamani, kiongozi wa chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF Debretsion Gebremichael. Vikosi vinavyomtii Debretsion vilichukua udhibiti wa mji wa Adigrat, ambao ni wa pili kwa ukubwa katika jimbo la Tigray. Wamewalaumu walio kwenye mamlaka kwa kuyarubuni maslahi ya Watigray.
Makamu wa rais katika utawala wa mpito kwenye eneo la Tigray nchini Ethiopia, Jenerali Tsadkan Gebretensae, amesema "wakati wowote vita kati ya Ethiopia na Eritrea vinaweza kuanza.” Gebratensae aliyasema hayo alipofanya mahojiano na Jarida linaloandika kuhusu maswala ya Afrika mnamo siku ya Jumatatu.
Wachambuzi wanasema mapigano ya moja kwa moja kati ya majeshi mawili makubwa kabisa barani Afrika yanaweza kuwa pigo kwa maelewano ya kihistoria yaliyosababisha Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel mnamo mwaka 2019.
Wachambuzi pia wanasema vita hivyo vikianza tena basi vinaweza kuyaingiza kwenye vita hivyo mataifa mengine yenye nguvu kwenye kanda hiyo.
Kjetil Tronvoll, profesa wa Chuo Kikuu cha Oslo anesema anahofia kwamba Eritrea ambayo ni mpinzani wa kihistoria wa Ethiopia huenda ikatumia mvutano huo kuanzisha hatua za kijeshi.
Wachambuzi wanasema kutoridhika kwa Rais wa Eritrea Isaias Afwerki na makubaliano ya amani ya mwaka 2022, matarajio ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed katika bandari ya Bahari Nyekundu na maslahi ya kisiasa za kikanda ya Mashariki ya Kati ni sababu zinazochochea mvutano na hali ya kuzorota kwa uhusiano kati ya Ethiopia na Eritrea.
Umoja wa Afrika (AU) kwenye taarifa yake umesema umekuwa ukifuatilia kwa karibu hali inayoendelea ndani ya chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF) kwa wasiwasi mkubwa.
Soma pia: Wanajeshi wa Eritrea waondoka Tigray
Balozi za nchi za Magharibi, ikiwa ni pamoja na Marekani, Uingereza, Japan na Umoja wa Ulaya zimetoa wito wa kufanyika "mazungumzo ya haraka" ili kupunguza mvutano.
Umoja wa Mataifa umesema unafuatilia kwa karibu matukio ya Tigray. Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric pia ametoa wito wa kufanyika "mazungumzo ya haraka" ili kuzuia nchi hizo zisirejee kwenye mzozo.
Vyanzo: AFP/RTRE