Kwa nini Trump ana hofu kubwa juu ya BRICS?
11 Julai 2025Rais wa Marekani Donald Trump ameapa kuongeza ushuru kwa mataifa yanayounga mkono mpango wa BRICS – jumuiya ya mataifa yenye uchumi unaokua kwa kasi – kwa kile alichokiita "sera za kuipinga Marekani.”
Ingawa BRICS bado haijafanikisha malengo makubwa, mvuto wake kwa mataifa kutoka Kusini mwa Dunia unaongezeka, hali inayozidisha wasiwasi wa Washington.
Katika kile kinachoonekana kama jaribio la kulinda nafasi ya dola kama sarafu kuu ya dunia, Trump alitishia Jumapili kuweka ushuru wa ziada wa asilimia 10 kwa bidhaa kutoka kwa mataifa yoyote yanayiounga mkono BRICS.
Hatua hiyo inakuja huku muda wa kusitishwa kwa ushuru mpya wa siku 90 ukitarajiwa kumalizika Jumatano hii, na Ikulu ya Marekani ikisema tayari imetuma barua kwa nchi kadhaa juu ya ushuru mpya.
Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, BRICS imekua kutoka wanachama 4 hadi 10, ikijumuisha Indonesia, huku Saudi Arabia ikiwa kwenye orodha ya wanachama ingawa haijathibitisha rasmi.
Licha ya maendeleo ya polepole, zaidi ya mataifa 20 yameonyesha nia ya kujiunga na umoja huo, ambao kwa sasa unawakilisha robo ya uchumi wa dunia na karibu nusu ya idadi ya watu duniani.
Kulingana na Alicia Garcia-Herrero kutoka taasisi ya Bruegel mjini Brussels, "Trump ana sababu ya kuwa na wasiwasi. BRICS inapingana waziwazi na mataifa ya Magharibi na inalenga kubadilisha mfumo wa dunia.”
BRICS imeongeza juhudi za kupunguza utegemezi wa dola kwa kuhamasisha biashara kwa sarafu za ndani. Russia na China zinaongoza harakati za "kuachana na dola," huku India ikilipa mafuta kutoka Russia kwa yuan, rubles na dirham ya Falme za Kiarabu.
Hata hivyo, mpango wa kuanzisha sarafu ya pamoja inayoungwa na dhahabu — "Unit" — umekwama kutokana na migongano ya ndani. India na Brazil zinapendelea biashara kwa sarafu zao kuliko kuunda sarafu mpya ya BRICS inayohofiwa kuwa na ushawishi mkubwa wa China.
Je, BRICS ni tishio halisi?
Kulingana na takwimu za mwaka 2024, BRICS ilihusisha asilimia 3 pekee ya jumla ya biashara ya kimataifa ya dola trilioni 33 — kiasi kidogo ikilinganishwa na uzito wa kiuchumi wa mataifa haya.
Dola ya Marekani bado inatumika katika karibu asilimia 90 ya miamala ya dunia na inahifadhiwa kwa asilimia 59 ya akiba ya fedha za kigeni duniani.
Wachumi kama Herbert Poenisch wanahisi kuwa kwa sasa "kuitikisa dola ni jambo gumu,” kutokana na udhibiti wa mtaji wa yuan, kuyumba kwa ruble, na kusuasua kwa baadhi ya wanachama wa BRICS katika kupunguza utegemezi kwa dola.
Kwa sasa BRICS inaendelea kupanuka, ikijumuisha wanachama wapya kama Ethiopia, Misri, Iran na Falme za Kiarabu. Wengine kama Algeria na Malaysia wako njiani kujiunga. Nchi nyingi zinavutwa na matarajio ya mfumo wa dunia usiotawaliwa na Magharibi.
Kwa mataifa kama Iran na Russia, BRICS ni tumaini la kujinusuru na vikwazo vya Magharibi kupitia mifumo mbadala ya malipo kama BRICS Pay na BRICS Bridge. Ethiopia na Misri kwa upande wao, wanatafuta msaada wa maendeleo bila masharti ya kisiasa kama ilivyo kwa misaada ya nchi za Magharibi.
Lakini Trump ameonya kuwa kujiunga na BRICS sasa kuna gharama. Garcia-Herrero anasema, "Gharama hii mpya inaweza kuwatisha hasa mataifa maskini.”
Pamoja na matumaini ya kiitikadi na kiuchumi, BRICS bado inakabiliwa na changamoto kubwa za mshikamano na mkakati wa pamoja. Mfano ni mpasuko kati ya India na China na kutotekelezwa kwa taasisi mbadala zenye nguvu. Benki ya Maendeleo ya BRICS (NDB) imetoa mikopo ya dola bilioni 39 pekee, ikilinganishwa na zaidi ya trilioni moja ya Benki ya Dunia.
BRICS inazidi kuwa kitovu cha siasa za dunia
Katika mkutano wao wa Brazil, viongozi wa BRICS walikosoa vikwazo vya upande mmoja na sera za ushuru wa kujilinda, wakisema vinapotosha biashara ya dunia na kukiuka sheria za WTO — ingawa hawakumtaja Trump moja kwa moja.
Pamoja na masuala ya uchumi, viongozi hao pia walijadili masuala ya usimamizi wa teknolojia ya AI, mabadiliko ya tabianchi na afya ya kimataifa. Walitoa msimamo mkali dhidi ya mashambulizi dhidi ya Iran na kutetea uhuru wa Palestina, huku wakikemea matumizi ya "njaa kama silaha” Gaza.
Hata hivyo, hawakumlaumu moja kwa moja Russia, na badala yake walilaani mashambulizi ya Ukraine dhidi ya miundombinu ya Russia, wakitoa wito wa "suluhu ya amani ya kudumu.”
Viongozi wa BRICS pia walisisitiza haja ya mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wakitaka mataifa kama Brazil, India na moja kutoka Afrika yapewe viti vya kudumu.
Ingawa Donald Trump anaendelea kupaza sauti dhidi ya BRICS, wachambuzi wengi wanasema umoja huo bado uko hatua za awali, na bado hauna uwezo wa kuipindua dola kama nguvu kuu ya kifedha duniani.
Hata hivyo, ukuaji wake wa haraka na ujumbe wa kuhamasisha mfumo wa dunia wenye usawa zaidi ni dalili kwamba Marekani haiwezi kupuuza mabadiliko yanayochipua.