Kuyumba kwa uchumi kunahatarisha malengo ya maendeleo 2030
17 Julai 2025Afrika Kusini ambayo ni mwenyekiti wa nchi zilizostawi na zinazoinukia kwa kasi kiuchumi duniani za G20, imetahadharisha kwamba kuwachana na mfumo wa kimataifa unaozingatia sheria na kupungua kwa ushirikiano huenda kukavuruga malengo ya maendeleo ya 2030 ya kutokomeza njaa, umaskini uliokithiri na kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Waziri wa Fedha wa Afrika Kusini, Enoch Godongwana amewaambia wakuu wa fedha wa nchi za G20 na magavana wa benki kuu kwamba wakati mfumuko wa bei unazidi kupungua hatua kwa hatua na hali ya kifedha ikiwa imeanza kutengemaa katika baadhi ya mikoa, hali ya kutokuwa na uhakika inaendelea kuelemea sana matarajio ya ukuaji uchumi wa kimataifa.
Pia amesema kuongezeka kwa vikwazo vya biashara, kukosekana kwa usawa wa kimataifa na vitisho vipya vya kijiografia vimeibua wasiwasi mkubwa.
Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent hahudhurii mkutano huo wa siku mbili katika mji wa bandari wa Durban, na Marekani badala yake inawakilishwa na naibu waziri wa masuala ya kimataifa.