“Ilikuwa Nzuri”: Barafu ya Mlima Kenya yatoweka kwa kasi
26 Machi 2025Charles Kibaki Muchiri, mwongozaji wa watalii mwenye uzoefu wa karibu robo karne, anaelezea kwa huzuni jinsi Mlima Kenya ulivyobadilika. Akiwa amezoea kupanda mlima huu wenye urefu wa mita 5,000 juu ya usawa wa bahari, Muchiri anakumbuka enzi za mapango ya barafu na tabaka nene la theluji lililodumu kwa miezi kadhaa.
Barafu ya Lewis Glacier, ambayo hapo awali ilikuwa ikifunika mteremko mmoja wa mlima, sasa imebakia vipande viwili vidogo tu – kikubwa kikiwa na upana wa mita chache.
Soma pia: Moto katika mlima Kenya
Uchunguzi wa kisayansi unaonyesha kuwa barafu hiyo imepungua kwa asilimia 90 kati ya mwaka 1934 hadi 2010. Utafiti mwingine wa hivi karibuni umeonesha kuwa barafu yote ya Mlima Kenya imebaki na eneo la asilimia 4.2 tu ya ilivyokuwa mwaka 1900.
Athari kwa mazingira, utalii na jamii
Mlima Kenya, ambao ni eneo la Urithi wa Dunia la UNESCO, huvutia maelfu ya watalii kila mwaka. Mandhari yake ni ya kipekee – kuanzia misitu minene ya tembo kwenye mwinuko wa chini hadi vilele vya miamba vinavyochomoza baada ya saa kadhaa za kupanda.
Lakini mabadiliko ya tabianchi yamesababisha kupungua kwa theluji, jambo ambalo linadhoofisha barafu kwa kukosa kinga dhidi ya jua kali. Baadhi ya njia maarufu za kupanda mlima ambazo zilihitaji barafu sasa hazitumiki tena. Aidha, mito inayotiririsha maji kutoka barafu hiyo inazidi kukauka, hali inayotishia uhai wa wanyama, mimea na wakazi wa vijiji vya karibu.
Wataalamu wa UNESCO wanasema kuwa barafu iliyobaki haina tena mchango mkubwa kwa mfumo wa maji, bali imebaki na umuhimu wa kihistoria na kielimu.
Je, barafu itakuwepo tena?
Juhudi zinaendelea kufanywa na vijana wa Kenya kupanda miti kwenye mteremko wa mlima kwa lengo la kurejesha mazingira na kusaidia kuhifadhi unyevunyevu. Lakini wataalamu kama Alexandros Makarigakis wanaonya kuwa juhudi hizo haziwezi kuzuia kile kilicho dhahiri – kwamba Mlima Kenya uko njiani kupoteza barafu yote.
"Muda si mrefu tutakuwa na kizazi ambacho hakiwezi kuihusisha Afrika na barafu,” alisema Makarigakis.
Mlima Kenya sio tu alama ya asili na urithi wa taifa, bali pia ni kielelezo cha athari halisi za mabadiliko ya tabianchi. Hatua za haraka za kimazingira na kisera zinahitajika ili kupunguza kasi ya uharibifu huu.
Chanzo: AFP