Kutoka Koblenz hadi Hindu Kush: Wasifu wa Fritz Urbach, mwanajeshi wa Kijerumani
8 Agosti 2011Watu wengi wanaizingatia tarehe 11 Septemba kuwa siku ya jaala, maana yaliyotokea siku hiyo nchini Marekani yameyabadili maisha ya watu duniani kote, akiwemo Kanali Fritz Urbach afisa wa Jeshi la Ujerumani, aliyepelekwa nchini Afghanistan mara tu baada ya mashambulizi ya siku hiyo kutekeleza jukumu la kuwazuia magaidi kupata mahala pa kujificha katika nchi hiyo. "Mimi sikuwa na uhakika iwapo picha nilizokuwa (kwenye televisheni) zilikuwa za kweli. Kwanza nilidhani kwamba hazikuwa halisi na sikuzielewa. Nilipokuja kuamini kuwa ni za kweli, ndipo mawazo yaliponijia na kujiuliza, je mambo haya yatakuwa na athari gani kwa nchi za Magharibi?" Anakumbuka Fritz.
Septemba 11 na wito wa mshikamano kwa mataifa ya NATO
Fritz amekuwa akilitumikia jeshi la Ujerumani tokea mwaka 1997. Siku hiyo yalipotokea mashambulio ya nchini Marekani, Fritz alikuwa na zamu ya ulinzi kwenye kambi ya jeshi katika mji wa Koblenz. Anakumbuka kuwa aliona katika televisheni jinsi jengo la Kituo cha Biashara Duniani (World Trade Centre – WTC) lilivyokuwa linawaka moto. Anasema hataisahau siku hiyo maishani mwake. Mashambulio haya ya kigaidi yalikuwa na maana ya kuimarisha moyo wa mshikamano na washirika wengine wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, ambayo Ujerumani na Marekani ni wanachama.
Miezi michache baadaye, jeshi la Ujerumani lilianza kuutekeleza uamuzi wa Bunge la Ujerumani juu ya kuyatimiza majukumu ya kimataifa. Kwa usemi mwingine, wanajeshi wa Ujerumani walipelekwa Afghanistan wakiwa katika operesheni ya pamoja na majeshi ya nchi nyingine za NATO yenye lengo la kulinda amani na kuleta utengemavu nchini humo.
Wakati huo Fritz alikuwa kamanda na alishiriki katika maandalizi ya kikosi cha kwanza kilichopelekwa Uturuki kwa ajili ya kupatiwa mafunzo ya kujitayarisha kwenda Afghanistan. Ni hapo ndipo alipotambua kuwa kumbe alichokuwa anakiona kwenye televisheni kilikuwa kitu halisi, maana sasa ilibidi aikimbie familia yake kwa mara ya kwanza. "Mke na watoto wangu, ambao walikuwa wadogo zaidi wakati huo, walijua tokea mwanzo kabisa kwamba nitapelekwa kufanya kazi Afghanistan. Lakini mke wangu wakati wote anayaelewa ninayoyafanya na aliniunga mkono katika kuyatimiza majukumu na wajibu wangu." Anasema Fritz.
Kutoka Ujerumani hadi Afghanistan
Hivi sasa Kanali Fritz Urbach anatoa mchango wake katika juhudi za kuijenga upya Afghanistan. Amefanya kazi katika mji mkuu Kabul na baadaye kaskazini mwa Afghanistan, ambako alikuwa kiongozi wa timu ya ujenzi ya jimbo la Feisabad. Ameshafanya kazi mara kadhaa katika maeneo ya milima ya Hindu Kush.
Kanali huyu anasema kwamba kuishi na kufanya kazi nchini Afghanistan ni kuwa tayari kukabiliana na hatari ana kwa ana. "Mashambulizi ya tarehe 15 Aprili 2010 yaliwauwa askari watatu waliokuwamo katika timu yangu ya ujenzi na kuwajeruhi wengine watano, baadhi vibra sana." Anakumbuka kwa masikitiko. Miongoni mwa majukumu ya Fritz yalikuwa ni kuwasimamia askari hao, kwa hivyo alikuwa ni yeye aliyelazimika kutoa habari kwa familia zao nyumbani na kuwahudimia kwa mambo mengine yote. Kabla ya mashambulizi hayo kutokea, Fritz aliagana na askari wenzake, kwa hiyo yaliyotokea yaliugusa moyo wake kwa ndani kabisa.
Tangu ipeleke wanajeshi wake nchini Afghanistan, Ujerumani imeshapoteza askari wake, na Fritz hana uhakika iwapo Afghanistan haitarejea tena kuwa kituo cha magaidi baada ya kuondoka kwa majeshi ya kimataifa. Hata hivyo, anasema kuwa sasa inapasa kuwapa watu wa Afghanistan uwezo kujilinda na kuweza kuwa na serikali yenye uhakika wa kuongoza. "Kama hatua hizo zitafikiwa, basi itawezekana kuwaachia Waafghani wajibu wa kuiendesha nchi yao".
Mwandishi: Daniel Scheschkewitz/ZPR
Tafsiri: Abdu Mtullya