Kurejea kwa Trump kwachochea taarifa potofu Afrika
20 Mei 2025Kurudi kwa Trump madarakani kwa mara ya pili kumechochea ongezeko la taarifa potofu kuhusu Afrika. Watafiti wanaonya kuwa hii ni ishara ya mabadiliko makubwa katika mitazamo ya mtandaoni yanayochochewa na migogoro ya kisiasa na ukosefu wa imani kwa vyombo vya habari vya kawaida.
Katika wiki za hivi karibuni, nchi tatu kubwa barani Afrika — Afrika Kusini, Nigeria na Kenya — zimejikuta katikati ya mzunguko wa propaganda na taarifa zisizo sahihi zinazohusishwa na Rais wa Marekani Donald Trump.
Afrika Kusini: ‘Mauaji ya wakulima weupe' yarejea
Afrika Kusini imekuwa shabaha ya kwanza ya shutuma kutoka kwa serikali mpya ya Marekani. Trump alidai kupitia mitandao ya kijamii kuwa serikali ya Afrika Kusini inachukuwa ardhi ya wakulima weupe bila fidia, jambo ambalo limekanushwa na wataalamu na maafisa wa serikali.
Sheria hiyo mpya, wanasema, inaruhusu unyang'anyi wa ardhi kwa fidia ya haki tu. Hata hivyo, Trump alichochea kile kinachojulikana kama nadharia ya "mauaji ya wazungu," akidai kuwa wakulima 60 weupe huuawa kila siku – madai ambayo yamepuuzwa na takwimu rasmi. Kwa mujibu wa Umoja wa Kilimo wa Transvaal, watu takriban 50 wa rangi zote huuawa kwa mwaka mashambani, na vifo vyote vya mashambani tangu miaka ya 1990 vimefikia karibu 3,000.
Mchambuzi Gideon Chitanga anasema matamshi hayo ni "mabaya na yenye madhara," kwani yanaweza kuchochea uhasama wa kidini na kikabila. Dkt Trust Matsilele, mhadhiri wa uandishi wa habari Uingereza, anasema Trump anasaidia kusambaza mitazamo potofu kwa faida ya kisiasa.
Nigeria: Siasa, AI na nadharia za msaada kutoka kwa Trump
Nchini Nigeria, wafuasi wa harakati ya kujitenga ya IPOB wametengeneza video bandia zinazoonyesha Trump na hata Rais wa Finland wakiunga mkono harakati zao. Mwanzilishi wa IPOB anakabiliwa na mashtaka ya uhaini.
Soma pia: Ukraine: Trump 'yuko katika ulimwengu wa upotoshaji', asema Zelensky
Pia, kuna madai ya kupotosha kuhusu kukatwa kwa misaada ya kigeni ya Marekani, huku video zenye uhariri wa dijitali zikitumika kudai kuwa viongozi wa Nigeria wamefukuzwa Marekani au kuzuwiliwa mali zao. Lanre Olagunju, mchambuzi wa taarifa na mhariri wa CheckClimate.Africa, anasema: "Trump ametumia mitandao ya kijamii kwa ufanisi mkubwa kuhalalisha taarifa potofu kama silaha ya kisiasa."
Kenya: Mgawanyiko wa ndani wazua mazingira ya propaganda
Nchini Kenya, video bandia kwenye mtandao wa TikTok zilimuonyesha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua — ambaye aliondolewa madarakani — akihudhuria kuapishwa kwa Trump. Pia, madai kuwa Kenya imejiondoa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) yaliibuka, yakitokana na video ya zamani ya daktari anayeeneza upotoshaji kuhusu afya.
Odanga Madung, mtafiti wa teknolojia na jamii, anaona kuwa kurudi kwa Trump kumewapa nguvu wafuasi wa siasa kali kote duniani. "Mashambulizi ya kidijitali dhidi ya vyombo vya habari yataongezeka kabla ya uchaguzi wa Kenya 2027," anasema Nyakerario Omari kutoka shirika la Code for Africa.
Soma pia: Upotoshaji wa mtandaoni wachochea hofu Kenya kuelekea uchaguzi
Kwa mujibu wa Chitanga, dunia inaingia katika enzi mpya ya mawasiliano ambapo "tunapaswa kuvumbua mbinu mpya za kuchuja taarifa potofu."
Mabadiliko haya ya kidijitali yanayoambatana na kurudi kwa Trump si ya kawaida. Taarifa potofu sasa zimekuwa silaha ya kisiasa, na Afrika imo kwenye msitari wa mbele wa mapambano haya ya ukweli dhidi ya propaganda.