Kurasa za magazeti ya Ujerumani
14 Juni 2006Ziara ya ghafla ya rais George W. Bush nchini Irak na marufuku ya matangazo ya biashara kwa sigara ndizo mada zilizohodhi vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani hii leo.
Amefika bila ya kutarajiwa na kukutana na waziri mkuu wa Irak Nuri el Maliki.Kiongozi huyo wa Marekani George W. Bush amesifu sera za serikali ya Irak.Ziara hiyo fupi na ya ghafla imewashughulisha pia wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.
Frankfurter Allgemeine linaandika:
“Hakuna shaka yoyote,uamuzi wa kumtembelea kwa muda mfupi na bila ya kutegemewa waziri mkuu wa Irak,El Maliki umelenga kushadidia maguvu ya nguvu ya rais Bush ,ndani na nje ya nchi yake.Lakini kama kupeyana mikono katika kasri la mjini Baghdad,ni mzigo kwa siasa ya ndani ya waziri mkuu El Maliki au la,hakuna ajuae,dhahiri ni kwamba na yeye pia anabeba dhamana ya usalama nchini humo.
Ndio maana,chambelecho, wanalazimika ,mrepublican Bush na mshiya El Maliki,kufa kupona, kushirikiana-wakifanikiwa ,kupanuwa eneo la usalama,pamoja na kuvunja nguvu machafuko ya waasi na makundi ya wanaharakati wa itikadi kali ya dini ya kiislam;wakifanikiwa kuwaokoa toka balaa la kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe washiya na wasunni,hapo ndipo kupeyana mikono viongozi hao wawili litakua jambo la maana.Bush ataweza kupunguza idadi ya wanajeshi wake bila ya kuonekana kana kwamba wanazipa kisogo dhamana zao,na wakati huo huo msimamo na madaraka ya El Maliki yatazidi kupata nguvu.”
Gazeti la OSTSEE-ZEITUNG la mjini Rostock linaleta uwiano wa ziara hii ya sasa ya Bush na ile aliyoifanya miaka miwili na anusu iliyopita nchini Irak.Gazeti linaandika:
“Ziara hiyo ya rais George W. Bush iliyovigutua vyombo vya habari-imefanyika katika hali tete sawa na ile iliyokuwepo alipofika kwa mara ya kwanza,na kwa muda mfupi pia nchini Irak November mwaka 2003.
Wakati ule George W. Bush aliweza kuwaahidi wanajeshi katika sherehe za “Kushukuria ”au “Thanks Giving” “Tutasalia hadi kazi itakapokamilika.”Hakuna uhakika kama ahadi hiyo itatekelezeka.Rais George W. Bush anajikuta anabanwa:-nyumbani umaarufu wake unazidi kuchujuka na siasa zake za kuwajibika kijeshi nchini Irak zinazidi kupingwa.
Mada nyengine magazetini inahusu marufuku ya matangazo ya kibiashara kwa sigara.
Kwa jumla wahariri wa magazeti wa Ujerumani wanahisi Ujerumani haina nafasi hata chembe ya kushitaki kwa lengo la kubatilisha uamuzi huo uliopitishwa na Umoja wa Ulaya. Mwanasheria mkuu anaeshughulikia suala hilo katika korti kuu ya Ulaya mjini Luxembourg ametetea umuhimu wa kufutiliwa mbali madai yaliyopelekwa mahamani tangu enzi za utawala wa Gerhard Schröder.
Gazeti la Tageszeitung la mjini Berlin linaandika:
„Marufuku ya matangazo ya biashara kwa sigara hayaepukiki.Wanaotaka kuyazuwiya wameondolewa patupu na mahakama ya ulaya mjini Luxembourg.Wanachokitaka hasa sio hoja kwamba muongozo wa Umoja wa ulaya katika suala la matangazo ya kibiashara umefurutu au la, bali kuhakikisha masilahi ya makampuni ya sigara ya Ujerumani yanalindwa.
Marufuku hayo yakianza kufanya kazi,itakua hasara kubwa kwa viwanda vya sigara.Kile ambacho kimsingi hakukua na haja ya kukipigia upatu,kinaingia njiani:bidhaa ambayo kila mwaka inaangamiza maisha ya watu milioni nne kote ulimwenguni,watu hawastahiki kuisifu kupitia matangazo ya kibiashara.