Ukandamizaji nchini Yemen unazorotesha misaada ya kiutu
3 Februari 2025Maamuzi yaliyochukuliwa na serikali ya Wahouthi nchini Yemen inayoungwa mkono na Iran yanaonesha kundi hilo liko kwenye mwelekeo usioeleweka. Alhamisi iliyopita wapiganaji wa Kihouthi waliwateka nyara wafanyakazi saba wa Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa.
Siku ya Ijumaa wanamgambo hao waliwaachia huru wafanyakazi 25 wa meli ya mizigo ya Galaxy waliyoiteka Novemba 2023. Mnamo siku ya Jumamosi wanamgambo hao pia waliwaachia huru wafungwa 153 wa kivita kwa mujibu wa shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu.
Kiongozi wa kundi hilo Abdul Malik al Houthi amesema hatua hizo zimechukuliwa kama juhudi za kuunga mkono makubaliano ya usitishaji vita huko Gaza. Hata hivyo kufikia wakati huu.
Wahouthi ambapo pia wanafahamika kama Ansar Allah bado hawajaweka wazi ni kwa nini hasa waliwateka nyara wafanyakazi hao saba wa Umoja wa Mataifa.
Soma pia:Marekani yalaani waasi wa Kihouthi kuwakamata wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa
Mtafiti mwandamizi kutoka kituo cha mafunzo ya kimkakati mjini Sanaa Abdulghani Al-Iryani ameiambia Dw kwamba, Wahouthi walifanya utekaji nyara huo kwasababu wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa ni watu muhimu na wanaweza kutumiwa kama karata ya kutafuta makubaliano.
Kwa upande mwingine mchambuzi kuhusu mgogoro wa Yemen Hisham Omeisy ambaye makao yake ni Washington nchini Marekani pia anaamini kwamba Wahouthi walihitaji karata mpya ili kupata fursa ya kufanya mazungumzo.
Omeisy ameiambia dw, kwamba wakati kundi hilo likiwa liko kwenye orodha ya kusubiri kuingizwa kwenye kundi la kitabu cha makundi ya kigaidi ya kimataifa na huku likiwa rasilimali zake zinazidi kupunguwa, limejikuta likihitaji kuchanga vizuri karata zao na kufanya kile ambacho wamekuwa wakikifanya vizuri siku zote, nacho ni kuendesha matukio ya utekaji nyara na kutumia nguvu.
Marekani yairejesha kundi la Wahouthi kwenye orodha ya magaidi
Pamoja na hayo ikumbukwe kwamba Saa chache baada ya kuapishwa madarakani Januari 20 huko Marekani, Donald Trump, alisaini amri ya kulirudisha tena kundi la Houthi katika orodha ya makundi ya kimataifa ya kigaidi kutokana na mashambulio yake iliyoyafanya dhidi ya meli kadhaa katika bahari ya Sham na dhidi ya Israel. Amri hiyo ya rais itaanza kutekelezwa ndani ya siku 30, ambayo kimsingi ni mwishoni mwa mwezi Februari.
Wahouthi wamekuwa wakiilenga Israel pamoja na safari za meli za kimataifa za usafirishaji mizigo kupitia bahari ya Sham katika kile ambacho wamekuwa wakikiita kuwa ni hatua ya kuinga mkono Hamas na Wapalestina katika kipindi cha miezi 15 ya vita vya Ukanda wa Gaza.
Soma pia:Waasi wa Houthi wa Yemen waachilia huru wafungwa wa kivita wapatao 153
Na mara kadhaa wamekuwa wakiahidi kusitisha hujuma zao pale yatakapofikiwa makubaliano ya kusitisha vita.
Na baada ya Israel na Hamas kufikia makubaliano hayo mwezi huu, hata hivyo Wahouthi wamesema bado wataendelea kuzilenga meli za Israel au zile zinazomilikiwa na Waisrael. Wanadai wataacha hujuma hizo pale itakapoanza awamu nyingine ya makubaliano ya usitishaji vita Gaza.