Hamas yasema iko tayari kwa mazungumzo na Israel
19 Machi 2025Kundi la wanamgambo wa Hamas limesema bado njia ya mazungumzo ya amani kati yake na Israel iko wazi na limetoa wito kwa Israel kutelekeleza makubaliano ya usitishaji wa vita yaliyotiwa saini Januari 19. Wito huo unafuatia hatua ya Israel kuyavunja makubaliano hayo na kuanzisha upya mashambulizi huko Gaza.
Mapema leo, Israel ilifanya mashambulizi katika Ukanda wa Gazana kuua watu 13 kwa mujibu wa shirika la ulinzi wa raia kwenye Ukanda huo.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema mashambulizi hayo ni mwanzo tu na kwamba wataendelea nayo hadi pale mateka waliochukuliwa na Hamas watakapoachiliwa.
Umoja wa Mataifa na mataifa mbalimbali duniani yamelaani idadi kubwa ya vifo vya raia katika mashambulizi hayo mapya, ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 400, kwa mujibu wa wizara ya afya ya eneo hilo inayosimamiwa na Hamas.
Hadi sasa mashambulizi ya Israel huko Gaza yamewaua zaidi ya watu 48,000 wengi wao wakiwa raia, kulingana na takwimu za wizara ya afya ya eneo hilo.