Hamas: Vikosi vya Israel viondoke kusini mwa Gaza
14 Machi 2025Msemaji wa Hamas, Hazem Qassem amesema wanajeshi wa Israel walipaswa kuondoka Kusini mwa Ukanda wa Gaza katika eneo ambalo ukanda huo unapakana na Misri. Amesema hatua hiyo ilitakiwa kuchukuliwa wakati wa awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha vita iliyoanza Januari 18.
Hamas imeishutumu Israel kwa kuendelea kuviweka vikosi vyake kwenye njia ya kimkakati ya Philadelphi. Israel yenyewe imesisitiza inahitaji kuidhibiti njia hiyo ili kuzuia silaha kupitishwa kwa njia za magendo ndani ya Gaza kutoka Misri. Kulingana na msemaji wa Hamas, njia ya Philadelphi imekuwa kizingiti katika mazungumzo ya usuluhishi yanayolenga kuingia katika awamu ya kusimamisha vita.
Soma zaidi: Hamas yasema iko tayari kwa awamu ya pili ya kusitisha vita
Awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusimamisha vita ilimalizika Machi mosi bila makubaliano ya hatua zinazofuata. Hayo yanajiri wakati waandamanaji wanaoshinikiza mateka waachiliwe wamefanya maandamano nje ya wizara ya ulinzi ya Israel jana Alhamisi kushinikiza yafanyike makubaliano ya kusitisha vita yatakayoruhusu mateka wote waliosalia waachiliwe katika awamu moja.
UN yaishutumu Israel kwa unyanyasaji wa kijinsia na kingono wakati wa vita Ukanda wa Gaza
Katika hatua nyingine, Umoja wa Mataifa katika tamko linaloungwa mkono na wataalamu wa haki za binadamu limeituhumu Israel kwa kufanya ukatili wa kingono na aina nyingine za kimfumo za unyanyasaji wa kijinsia, wakati wa vita vyake dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Shutuma hizo zilizotolewa Alhamisi zimewasilishwa katika ripoti iliyoandikwa kwa mapana kuhusu shambulio lililofanywa na wanamgambo wa Hamas kusini mwa Israel Oktoba 7 mwaka 2023.
Matokeo ya utafiti uliofanywa na Tume ya uchunguzi ya Shirika la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa unadhamiria kuhifadhi katika kumbukumbu shutuma na ushahidi wa uhalifu ili kuwawajibisha wahusika yanaweza kutumiwa na waendesha mashtaka wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC katika juhudi za kutoa haki kwa waathiriwa wa ukatili huo na familia zao.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ameikosoa vikali ripoti hiyo akisema tume ya wachunguzi huru iliyofanya utafiti huo imeendeleza chuki dhidi ya Israel ambayo imedumu kwa muda mrefu.